Tuesday, September 10, 2013

MCHANGO WA MZEE NGURUMO KWENYE SANAA YA MZIKI NCHINI WATAMBULIKA RASMI NA SERIKALI

11_fb546.jpg
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni, Bibi. Lilly Beleko kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo akimkabidhi Mzee Muhidini Gurumo barua kama ishara ya Serikali kutambua mchango wake uliotukuka katika tasnia ya Muziki nchini pamoja na kumpongeza kwa kustaafu kazi kazi hiyo, hivi karibuni nyumbani kwake Makuburi, Jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia nyuma ya Mkurugenzi ni Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Bw. Addo Mwasongwe na kulia pembeni ya Mzee Gurumo ni Mkewe, Bibi. Pili Said Kitwana.
22_c71f0.jpg
Nguli wa Muziki wa Dansi, Mzee Muhudini Gurumo (aliyevaa shati la drafti) akiwa na watumishi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, walipomtembelea nyumbani kwake Makuburi Jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Serikali kupitia Wizara hiyo ilimkabidhi barua rasmi Mzee huyo kutambua mchango wake katika tasnia ya Muziki na kumpongeza kwa kustaafu kazi hiyo. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni, Bibi Lilly Beleko, wa pili ni mke wa Mzee Gurumo, Bibi. Pili Said Kitwana na wa Pili Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara Upande wa Sanaa, Bibi. Joyce Hagu.(P.T)
Picha zote na Concilia Niyibitanga
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imempongeza Mzee Muhidini Gurumo kwa mchango wake uliotukuka katika tasnia ya Muziki nchini pamoja na kumpongeza kwa kustaafu kazi hiyo.
Akiwasilisha barua ya Serikali ya kutambua mchango wa nguli huyo juzi nyumbani kwake Makuburi Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bibi. Lilly Beleko amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wake katika muziki wa Dansi hapa nchini.
'Serikali inathamini mchango wako katika Muziki hapa nchini na itaendelea kuzienzi kazi hizo na inakupongeza kwa kazi nzuri ulioifanya ya kuelimisha, kuhamasisha na kuburudisha jamii'. Amesema Bibi. Beleko.
Naye Rais wa Shirikisho la Muziki nchini, Bw. Addo Mwasongwe, amesema kuwa Shirikisho linampongeza kwa kazi zake nzuri na litaendelea kumtumia katika kazi za muziki ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri katika tasnia hiyo.
Nguli huyo wa muziki wa dansi nchini katika enzi zake za uimbaji ametunga nyimbo za kuelimisha jamii kufanya kazi kwa bidii, kudumisha usawa, amani na kuwakumbusha wazazi kutimiza wajibu wao wa kuwalea watoto katika maadili mema.
Mzee Gurumo ambaye ameanza kazi ya muziki mnamo miaka ya 1960 na kustaafu kazi hiyo mwaka huu amesema kuwa anaishukuru Serikali kwa kutambua kazi yake na amefarijika kwa kukabidhiwa barua ya kumtambua na kumpongeza kwa kustaafu kazi hiyo.

No comments:

Zilizosomwa zaidi