Sunday, September 15, 2013

JESHI LA RWANDA LASOGEZWA MPAKANI...MAJESHI YA SADC YAENDELEA KUJIWEKA TAYARI KWA LOLOTE

Vikosi vya wanajeshi vya Serikali ya Rwanda vyenye silaha za kivita, sasa vimesogezwa katika eneo la mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Taarifa ya kusogezwa kwa vikosi hivyo mstari wa mbele katika eneo la mpakani, imetolewa jana na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Katika taarifa yake hiyo, SADC imeeleza wasiwasi wake kuhusu hatua ya Rwanda kusogeza mbele vikosi vyake vya kijeshi vilivyo na zana za kivita kwenye mpaka wake na Kongo.

Mshtuko huo wa SADC umekuja ikiwa ni siku chache tangu  MTANZANIA Jumatano iripoti kwa mara ya kwanza juu ya kuwapo kwa taarifa za Jumuiya hiyo kutuma ujumbe wa onyo kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda kuachana na fikra zozote mbaya dhidi ya Tanzania.

Onyo hilo, lilitolewa baada ya kupatikana kwa taarifa kuwa Serikali ya Kigali ilikuwa imepeleka vikosi vyake katika mpaka wake na Kongo, kwa ajili ya kupambana na waasi.

Ni hatua hiyo ya Serikali ya Kigali ndiyo iliyoilazimu SADC kutuma ujumbe mkali wa kumuonya Kagame kupitia kwa mmoja wa mawaziri wa nchi yake, aliyekuwa ameambatana naye kwenye mkutano wa viongozi wa nchi za Maziwa Makuu uliofanyika hivi karibuni nchini Uganda, ambao pia ulihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete.

Ikiwa ni takribani wiki moja baada ya kupatikana kwa taarifa za kutolewa kwa onyo hilo, jana mtandao wa Fox news ulikariri taarifa mpya ya SADC kupitia moja ya chombo chake, ikieleza kuzuka kwa hali ya wasiwasi baada ya kubainika kuwa Rwanda imeviamuru vikosi vyake vya jeshi kusogea eneo la mpaka wake na Kongo.

Ikitumia maneno ya kidiplomasia lakini yenye taswira ya kuonya, SADC kupitia taarifa yake hiyo iliyotolewa katika mkutano wake uliofanyika Namibia na kuhudhuriwa pia na Rais wa Kongo, Joseph Kabila, ilisema kuwa haifikirii kama Rwanda itajaribu kuivamia Kongo.

Taarifa hiyo inaitaka Rwanda kushiriki kuleta amani, usalama na utulivu ndani ya Kongo.

Katikati ya wiki hii, gazeti  la MTANZANIA Jumatano likikariri chanzo kimoja cha habari kilichokuwa kwenye mkutano wa viongozi wa nchi za Maziwa Makuu uliofanyika Uganda, kuwa ujumbe wa SADC kwa Rwanda alipatiwa mmoja wa Mawaziri aliyekuwa ameambatana na Rais Kagame muda mfupi baada ya kukutana na Rais Kikwete.

“Uamuzi wa Tanzania na Afrika Kusini kupeleka majeshi DRC, ni msimamo wa pamoja wa SADC. Vitisho vyovyote dhidi ya Tanzania au uvamizi wa kijeshi utachukuliwa ni uvamizi dhidi ya SADC, hivyo tutakuwa tayari kuingia vitani kupigana upande wa Tanzania.”

Hatua hiyo ya SADC kuikamia Rwanda, ilithibitishwa na taarifa ambazo gazeti hili liliziona kwenye mtandao wa Intaneti kupitia gazeti la The Namibian la nchini Namibia, ambalo liliandika kuwa, Jeshi la nchi hiyo (NDF), ambalo pamoja na majeshi ya nchi nyingine wanachama linaunda kikosi maalumu cha Jeshi la SADC, lilikuwa limeanza kushiriki mazoezi ya Jangwani karibu na Walvis Bay, yatakayodumu hadi Oktoba 15 mwaka huu.

Ilielezwa kuwa wakati mazoezi hayo yakiendelea, Mkuu wa majeshi ya Namibia (NDF), Luteni Jenerali, Epafras Ndaitwah, aliwakumbusha wapiganaji hao kuwa kwa sasa wanachama wenzao, wakiwemo wanajeshi wa Tanzania, wanapambana na maadui wa amani nchini Kongo na kwamba nao ni lazima wajiandae kwa hali yoyote ambayo haitabiriki.

Vikosi vya Kongo, vinavyoungwa mkono na vile vya Umoja wa Mataifa vilianzisha mapambano mapya dhidi ya waasi wa M23 mwishoni mwa mwezi uliopita huko Kaskazini Mashariki mwa Kongo.

Baada ya kupigana kwa mafanikio makubwa, SADC ilivipongeza vikosi vya Serikali ya Kongo na Brigedia inayoongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ya FIB kwa kuendelea kutumia shinikizo la kijeshi dhidi ya waasi wa M23 na vikosi vingine vilivyoko Mashariki mwa Kongo.

Tanzania, Malawi na Afrika Kusini, kwa pamoja zimetoa majeshi yao yanayounda brigedia ya wanajeshi wapatao 3,000 waliopewa mamlaka ya kupambana na vikosi vya waasi kwa kutumia nguvu.

Nchi zote hizo tatu zilikuwa zikiwasilishwa katika mkutano huo uliofanyika nchini Namibia.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukiishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo nchi hiyo imekuwa ikiyapinga.

Hata hivyo, waasi hao katika kujibu mashambulizi wamekuwa wakilishutumu Jeshi la Kongo kwa kuunganisha nguvu na kikundi cha waasi cha Kihutu cha FDLR, kinachopambana kutoka Mashariki mwa Kongo ambapo wanajeshi wake wengi wanaounda kikosi hicho, wanadaiwa kukimbia mauaji ya halaiki ya Rwanda yaliyotokea mwaka 1994.

Mazungumzo kati ya waasi na Serikali ya Kongo yalianza tena tangu Jumanne, baada ya kukwama mwezi Mei, kabla ya kuanza tena sasa baada ya kuibuka mapambano.

Wakati huo huo, juzi bomu dogo lililorushwa mjini Kigali liliua mtu mmoja na kujeruhi wengine 14 zikiwa zimesalia siku mbili tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa wabunge.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Rwanda, Damas Gatare alisema bomu hilo lilirushwa saa 12:30 jioni, katika eneo la sokoni lenye watu wengi.

Gatare alisema kuwa watu watatu wamekamatwa kutokana na tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea.

Hakuna yeyote anayeshutumiwa katika shambulio hili la sasa, lakini katika matukio mengine mawili kama hayo yaliyotokea mwezi Machi na Julai mwaka huu Serikali imekuwa ikilishutumu kundi la waasi wa FDLR kuhusika.

Rwanda inatarajia kufanya uchaguzi wa wabunge kesho, uchaguzi ambao unatarajiwa kutawaliwa na chama tawala cha Rais Kagame cha Rwandan Patriotic Front (RPF).

Chanzo-Mtanzania

No comments:

Zilizosomwa zaidi