Itatiro na maofisa wanne wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa walituhumiwa mwaka jana kuidhinisha kuchota kiasi hicho cha fedha bila ya kuwapo kwa ziara ya Rais kwenda nchi yoyote ya kigeni.
Mpango huo unadaiwa kusukwa Juni mwaka jana kwa maofisa haokuitaka Wizara ya Fedha kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya safari hewa ya Rais.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Juma Mahadhi alitoa maelezo hayo baada ya kuulizwa swali na Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge, Edward Lowassa.
Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli aliuliza swali hilo ghafla kwa Mahadhi wakati akitoka nje, baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati yake kilichofanyika kwenye ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam.
Mahadhi, ambaye alilazimika kutoa ufafanuzi wa swali hilo baada ya kubanwa zaidi na waandishi wa habari, alisema Rais Kikwete ndiyo mwenye mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya Itatiro kutokana na ripoti ya uchunguzi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkaguzi wa Ndani wa Wizara hiyo.
Alisema pia kuwa walishauriwa kuwa maofisa walioshirikiana na Itatiro nao wachukuliwe hatua za kinidhamu kufuatia njama hizo.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Katibu Mkuu Ombeni Sefue hakupokea simu. Pia hakujibu pindi alipotumiwa ujumbe mfupi kwa njia ya simu. Naye Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais anayeshughulikia Utumishi, George Yambesi alisema hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwani alikuwa likizo.
Mahadhi alisema wakati tukio hilo linatokea viongozi wakuu wa wizara hiyo walikuwa kwenye majukumu mengine ya Serikali, jambo ambalo lilisababisha nafasi zao kukaimiwa na watendaji hao.
“Wale maofisa walitumia mwanya wao wa kukaimu nafasi ile ndiyo wakasuka mpango huo,” aliongeza Mahadhi.
Alisema kutokana na hali hiyo baadhi ya maofisa hao wamechukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo ya kuwashusha vyeo na kuwabadilisha vitengo.
Mahadhi alisema kwamba huwa ni utaratibu wa kawaida kwa Rais anaposafiri maofisa wa Itifaki na wale wa Wizara ya Mambo ya Nje kupewa fedha na hazina kwa ajili ya kufanikisha ziara zake.
Chanzo: Mwananchi.
No comments:
Post a Comment