Monday, January 14, 2013

MAUAJI YA ALBINO YAIBUKA TENA TANZANIA...

    (Mary Owido mlemavu wa ngozi akiwa na watoto wake)
 
Walemavu wa ngozi nchini Tanzania yaani albino wamesema kuwa kumeibuka mbinu mpya zinazotumiwa na makundi ya watu wanaotumia kigezo cha kufunga ndoa na watu wa jamii hiyo na baadaye hutekeleza azma yao ya kuwaua na  kukata viungo vyao.

Kauli hiyo imetolewa na chama cha maalibino nchini Tanzania wakati walipokutana na waandishi wa habari kuelezea hali mpya ya wasiwasi inayowaandama watu wenye ulemavu wa ngozi nchini humo.

Huku wakielezea kuzorota kwa ulinzi na usalama, jamii hii ya walemavu wa ngozi  imesema kuwa serikali haijachukua hatua madhubuti kakabiliana na wimbi la matukio hayo ya kikatili ambayo pia yanahusishwa na imani za kishirikina.

Wale wanaoamini nguvu za kishirikina wamekuwa wakiviwinda viungo vya walemavu wa ngozi katika kile kinachoaminika kuwa  viungo hivyo vina nyota muhimu inayoweza kuwasaidia watu hao kupata utajiri wa mali.

Tangu kuzukwa kwa imani hiyo, mamia ya watu wenye ulemavu wa ngozi wamepoteza maisha wengine wakisababishwa ulemavu wa viungo na wengine kupoteza ndugu na familia zao.

Wakati matukio ya uvamizi na mashambulizi yakipungua kiasi  lakini kumeibuka mbinu mpya ambayo hutumiwa na wajanja wachache kuwarubuni wale wenye  ulemavu wa ngozi kwa minajili ya kufunga nao ndoa lakini baadaye ndoa hiyo hugeuka shubiri.

Wachambuzi wa mambo ya kijamii wanasema kuwa  serikali bado haijapiga hatua kubwa kuwahakikishia amani watu wenye ulemavu wa ngozi na pia huduma zinazotolewa kwao bado ni za kiwango cha chini.

No comments:

Zilizosomwa zaidi