Tuesday, January 15, 2013

AJARI YA TREN MISRI YAUA 19

Treni hii ilikuwa imewabeba makurutu wa jeshi
Treni ya kijeshi iliyokuwa imebeba makurutu wa jeshi imeanguka Kusini mwa Misri na kuwaua watu 19 na wengine zaidi ya miamoja kujeruhiwa.
Treni hiyo ilikuwa inaelekea katika kambi ya kijeshi mjini Cairo wakati behewa moja liling'oka na kuangukia treni moja ya mizigo katika eneo la Badrashin mjini Giza.
Waziri mkuu alitembelea eneo la ajali lakini aliokolewa na maafisa wake wa usalama baada ya watu walioshuhudia tukio hilo kumzomea.
Barabara za Misri pamoja na njia zake za reli zina rekodi mbaya sana ya usalama.
Mwezi Novemba mwaka jana watoto walifariki wakati treni walimokuwa wanasafiria ilipogongana na basi lao.
Waziri wa usafiri pamoja na mkuu wa mamlaka ya reli, walilazimika kujiuzulu kufuatia ajali hiyo.
Ghadhabu zimekithiri dhidi ya serikali kwa kukosa kuimarisha usalama wa usafiri wa reli pamoja na miundo msingi mjini Misri.
Watu walioshuhudia ajali ya leo walimzomea waziri mkuu Hisham Qandil wakisema ana damu mikononi mwake kwa kutokea ajali hiyo.
Ripoti zinasema kuwa zaidi ya abiria 1,300, walikuwa kwenye treni hiyo wakati ilipoanguka subuhi ya kuamkia leo.
Mmoja wa walioshuhudia ejali yenyewe alisema kuwa majeruhi walikuwa wamenaswa kwenye vifusi na kwamba magari ya Ambulance hayakuwasili hadi baada ya nusu saa. Miili ilikuwa imetapakaa kila mahali. Usaidizi uliweza kuwafikia tu baada ya saa moja.
Duru zinasema kuwa ajali hii inaweza kuongeza shinikizo dhidi ya serikali kuimarisha usalama wa usafiri wa treni
Miaka minne iliyopita watu kumi na nane waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika ajali ya treni mbili zilizogongana katika eneo la Giza.
Na mnamo mwaka 2002, treni nyingine iliteketea mjini Cairo, na kuwaua watu 373.

No comments:

Zilizosomwa zaidi