WATU saba wamekufa na wengine zaidi ya 47 kujeruhiwa vibaya
kwenye ajali iliyohusisha mabasi mawili yaliyogongana uso kwa uso katika
barabara kuu ya Mwanza-Musoma, wilayani Bunda mkoani Mara.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Mara, Absalom Mwakyoma, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 11:00
jioni, katika Kijiji cha Nyatwali, mpakani mwa Wilaya ya Bunda na mji
mdogo wa Lamadi, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Mwakyoma alisema ajali hiyo ilihusisha basi la Mwanza Coach lenye
namba T 736 AWJ na Best Line lenye namba 535 AJR, na kwamba chanzo cha
ajali hiyo ni mwendo kasi wa madereva wa mabasi hayo.
Alisema kuwa watu sita walikufa papo hapo na mmoja alifia katika
Hospitali ya Wilaya ya Bunda na kwamba madereva wa mabasi yote mawili
walitoroka baada ya ajali hiyo kutokea.
Aliwataja marehemu waliotambuliwa hadi sasa kuwa ni Amina Juma (35)
mkazi wa jijini Mwanza, Grace Mlimwa (50), mkazi wa Bunda na Magori
Ibrahimu (23) mkazi Bunda.
Alisema kuwa basi la Mwanza Coach lilikuwa linatokea mkoani Mara,
likielekea jijini Mwanza wakati Best Line lilikuwa linatokea jijini
Mwanza kuelekea Sirari, wilayani Tarime.
Aidha, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk. Rainer Kapinga alisema kuwa
wamepokea miili ya watu sita wakiwa ni wanawake watatu na wanaume
watatu na kwamba majeruhi mwingine alikufa baada ya kufikishwa
hospitalini hapo.
Alisema kuwa majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo ni 47, ambapo
wanane kati yao wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando
jijini Mwanza kutokana na hali zao kuwa mbaya.
|
No comments:
Post a Comment