
Serikali ilipotangaza rasmi kwamba Nyerere hatunaye tena, uchungu na simanzi uliikumba nchi nzima na dunia kwa ujumla hususani kwa wale waliokuwa wanamjua Nyerere na kujua alichokuwa akikisimamia na alichokiamini. Bara la Afrika likawa limempoteza kipenzi chake, mtoto wa Afrika ambaye thamani ya mchango wake katika ukombozi wa bara la Afrika haina kipimo. Mpaka anafariki dunia alikuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha amani barani Afrika.Mfano mzuri ni mgogoro wa Burundi aliokuwa akijaribu kuusuluhisha. Mwenyewe aliwahi kutamka kwamba yeye ni mwafrika kwanza na kisha mjamaa.
Mpaka leo hii jina la Nyerere linabakia kuwa kitambulisho chetu kikubwa .Wakati mwingine zaidi hata ya jina la nchi yetu yaani Tanzania.Wapo watu wanaolijua jina la Nyerere na wala wasijue jina la Tanzania au hata Tanganyika. Haishangazi, alikuwa ni mwana wa Afrika kamili. Kadiri siku zinavyopita, taratibu baadhi yetu, hususani vijana wanaoitwa wa kizazi kipya, wanazidi kulisahau jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Viongozi wetu wengi wa sasa( ingawa wakati wa msiba wake waliahidi kumuenzi kwa hali na mali) wanaelekea kusahau kabisa ahadi zao! Wengi wanabakia kumuenzi kwa maneno na sio vitendo.
Lakini je,sote tunafahamu japo kidogo tu historia ya Mwalimu Nyerere? Uwezekano ni kwamba sio wote,hususani vijana wa sasa. Kwa kifupi na kwa msaada wa vyanzo mbalimbali hii hapa historia fupi ya Hayati Baba wa Taifa;

Hayati Baba wa Taifa akisisitiza jambo
Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere alizaliwa tarehe 13 Aprili mwaka 1922 huko
Butiama mkoani Mara, pembezoni mwa ziwa Victoria,kaskazini mwa Tanzania.
Baba yake alikuwa ni Chifu katika kabila dogo la Wazanaki.Nyerere
alikuwa miongoni wa watoto wanaosemekana kufikia hadi 26. Baba yake,
Mzee Burito Nyerere alikuwa na wake wapatao 22.Alianza shule akiwa na
umri wa miaka 12 (ilimbidi kutembea kwa zaidi ya kilometa 26 hadi Musoma
mjini ili kupata elimu ya msingi). Kipaji cha uelewa shuleni
kilimuwezesha kumaliza kozi ya miaka minne ndani ya miaka mitatu tu.
Baadaye mnamo mwaka 1937,alijiunga na shule ya sekondari ya serikali ya
Tabora kwa masomo ya sekondari. Alibatizwa katika kanisa katoliki akiwa
na umri wa miaka 20.Kipaji chake cha kitaaluma na kiuongozi kilionekana tangu mapema. Kwa msaada wa waliokuwa waalimu wake pale Tabora (ma-father wa kanisa katoliki) baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda kusomea ualimu. Fikra za kimapinduzi na kusaidia waafrika wenzake zilianza kuonekana wazi akiwa Makerere.

Nyumba aliyojengewa Mwalimu Nyerere na serikali baada ya kustaafu.Ipo Butiama.
Baada
ya kumaliza Makerere alirejea Tanzania na kwenda kufundisha (St. Mary’s
Secondary School) mkoani Tabora. Mwaka 1949 alipata scholarship kwenda
Chuo Kikuu cha Edinburgh kusomea shahada ya pili (Masters) katika
historia na uchumi wa kisiasa(History and Political Economy). Alipokuwa
masomoni Edinburgh, Nyerere ndipo alipoanza rasmi kuunda mawazo yake ya
kiukombozi kufuatia kuanza kujifunza kilichoitwa Fabian Thinking .
Mawazo yake ya kuunganisha ujamaa na ujima au maisha ya kijamii ya
kiafrika ndipo yalipoanza kujijenga au kujiimarisha.Harakati za
kujipatia uhuru kwa nchi ya Ghana zilizokuwa zikiongozwa na Dr.Kwame
Nkrumah,anakiri Nyerere katika baadhi ya mahojiano aliyowahi kufanya,
zilichangia kuamsha fikra za kujikomboa kutoka mikononi mwa wakoloni. Inasemekana
Nyerere ndio alikuwa mtanzania wa kwanza kusomea katika chuo kikuu cha
Uingereza na mtanzania wa pili kupata degree nje ya Afrika. Alihitimu
mwaka 1952.
Mwalimu Nyerere na mkewe Mama Maria Nyerere.
Aliporejea
nchini Tanzania (enzi hizo bado ikiitwa Tanganyika), alianza kazi ya
kufundisha masomo ya Historia, Kiingereza na Kiswahili katika shule ya
St.Francis’ (sasa Pugu Sekondari). Wakati huo huo akawa amechaguliwa
kuwa mwenyekiti wa TAA(Tanganyika African Association) chama kilichokuwa
kimeundwa kusimamia maslahi ya waafrika ingawa tayari kikiwa na
vuguvugu la kiukombozi na kisiasa. Hapo ndipo serikali ya kikoloni
ilipomlazimisha kuchagua kati ya kufundisha(ualimu) au siasa. Mwenyewe
anasema alikuwa amepanga kufundisha kwa angalau miaka mitatu kwanza
kabla ya kuingia moja kwa moja kwenye siasa. Hilo halikuwezekana.
Akachagua kuwa mwanasiasa na hivyo kuanza mkakati mzito wa kuviunganisha
vyama mbalimbali vilivyokuwa na malengo sawa.
Mwalimu Nyerere ndani ya Butiama.
Kazi
ya kuviunganisha vikundi mbalimbali vya kisiasa vilivyokuwa vimeanza
kutapakaa nchi nzima haikuwa rahisi. Lakini alifanikiwa kufanya hivyo
mwaka 1954 kwa kuundwa kwa TANU(Tanganyika African National Union) na
yeye kuchaguliwa kukiongoza.
Humo ndimo alimopumzika Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.Tizama na tafakari kwa makini maneno yaliyoandikwa hapo nje.
Aliingia
katika bunge la wakati huo mwaka 1958 kabla hajawa waziri mkuu mwaka
1960. Tarehe 1 May 1961, Tanganyika ilipewa uhuru wa kujitawala na
Nyerere akawa waziri mkuu wa kwanza. Uhuru kamili ulipatikana mwaka
tarehe 9 December 1961. Mwaka mmoja baadaye (1962) Nyerere akawa Raisi
wa kwanza wa Tanganyika ilipokuwa Jamhuri ya Tanganyika.
Mwalimu Nyerere(katikati),mama yake
mzazi(kushoto) na mkewe Maria(kulia).Picha hii ilipigwa Novemba 10,1985
Butiama baada ya Nyerere kustaafu.
Julius
Nyerere alimuoa Maria Gabriel Magige (Mama Maria Nyerere) tarehe 24
Januari 1953 na walijaliwa kupata watoto wanane. Alipostaafu nafasi yake
ya uraisi mwaka 1985 alirudi kijijini Butiama ambako alibakia kuwa
mkulima wa kawaida mpaka kufariki kwake Oktoba 14, 1999. Endelea
kupumzika kwa amani Mwalimu.
Sura ya Nyerere katika noti ya Shs 100 enzi hizo.

R.I.P MWALIMU JULIUS K.NYERERE.
No comments:
Post a Comment