Monday, August 11, 2014

UKAWA WATABIRIWA KUMEGUKA VISIWANI ZANZIBAR



Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha UDP, Zanzibar, Juma Khamis Faki, ametabiri mgawanyiko na  kusambaratika kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Faki ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, aliyasema hayo wakati wa mahojiano maalum na NIPASHE wakati alipozungumzia tukio la baadhi ya wajumbe wa kundi la Ukawa kurejea bungeni.

“CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema kwa pamoja waliweka msimamo mkali dhidi ya kujihusisha na shughuli za bunge hili, ni wajibu wa kila chama kudhibiti wanachama wake, sasa Said Arfi, John Shibuda na Leticia Nyerere wote wa Chadema wamerudi bila shaka vyama vingine havitaafiki makubaliano wanayojiwekea” alieleza Faki.

Kwa mujibu wa maelezo yake, kuna matarajio makubwa kwamba wajumbe zaidi kutoka kundi linalounda Ukawa, watatinga bungeni wiki ijayo na kuendelea na majukumu yao.
Alisema hilo likitimia hususan kwa upande wa wana umoja huo kutoka CUF litasababisha mtikisiko wa kisiasa wa aina yake.

Aliongeza kuwa jambo pekee linaloonekana kuweza kurejesha utulivu wa hali ya hewa kwa upande wa Ukawa, ni kuwafukuza uanachama wajumbe hao ingawa alisema nalo linaweza kuwa gumu kwa Chadema, kwa kuwa siyo kazi rahisi kufukuza wajumbe watatu kwa mkupuo, ambao ni wabunge.

“Kama hawatawafukuza hao, kuonyesha msimamo wa mkakati wao Jumatatu nakuhakikishia wanachama wa NCCR-Mageuzi na CUF tutakuwa nao kwenye kamati za Bunge Maalum.”

Aliongeza kuwa kwa upande mwingine tendo hilo la kufukuza wabunge watatu kwa mkupuo litaigharimu Chadema kisiasa.

Hata hivyo, Faki alishauri Ukawa warudi bungeni  ili watekeleze majukumu yao watakaposhindwa kufanikiwa kutetea wanachoamini kuwa ni matakwa ya wananchi, ndipo wakashitaki kwa wananchi kilichowakwamisha.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Zilizosomwa zaidi