Sunday, May 26, 2013

WATU 5 WAPOTEZA MAISHA NA WENGINE 6 KUJERUHIWA KATIKA AJALI YA BASI LA SUPPER CHAMPION

Watu watano wamekufa papo hapo na wengine sita wamejeruhiwa, watatu wakiwa katika hali mbaya baada ya basi la Super Champion kugongwa na lori la mafuta eneo la Silwa, barabara ya Dodoma-Morogoro, mkoani Dodoma jana.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, David Misime amesema kwamba maiti mmoja alitambuliwa baada ya kukutwa na kitambulisho kilichoandikwa Raheli  Michael Masumbigana,  cha shule ya sekondari ya Mloa Barabarani.

Kamanda huyo alisema kwamba dereva wa lori hilo aina ya Scania lenye namba ya usajili  T 912 CAM likivuta tela T 494 BDG, Innocent Kangawe (37) mkazi wa Nkuhungu mkoani Dodoma anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano.

Kamanda Misime amesema kwamba majeruhi wamekimbizwa hospitali ya Gairo: “Ninaelekea huko kuwaona majeruhi," alisema Kamanda wakati wa mazungumzo na mwandishi kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio.

Ajali hiyo iliyotokea saa 7.15 mchana  inaonekana ilisababishwa na lori ambalo lilihama kutoka upande wake na kuingia upande wa kulia na kuligonga basi hilo T 277 AJR lililokuwa linaendeshwa na Twalib Issa (39) mkazi wa Chamwino Dodoma kuanzia ubavuni mbele hadi nyuma.

Lori hilo la mafuta ni mali ya kampuni ya Salmana Transport.

No comments:

Zilizosomwa zaidi