Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, limemkamata mkazi wa
Vijibweni, Said Tindwa kwa kosa la kufanya biashara ya dawa za kulevya
aina ya cocaine na heroine.
Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema mtuhumiwa huyo
ambaye ni mlemavu anayetumia mguu bandia, amekuwa akiutumia vibaya kwa
kuficha dawa ndani yake na kuwauzia watumiaji.
Alisema mtuhumiwa huyo aliweka dawa hizo kwenye pakiti na kuziuza sehemu mbalimbali kwa Sh1,000.
“Tulimkamata Agosti 2 mwaka huu katika mtego maalumu uliowekwa na askari wa upelelezi,” alisema Kova.
Alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu hiyo kwa muda mrefu kabla ya kukamatwa.
Kova alisema dawa alizokuwa akiuza mtuhumiwa ni zile za viwandani kama cocaine, heroine na bangi.
Wakati huohuo, polisi wanamshikilia askari polisi aliyerusha bomu la
machozi, Mbagala Zakhiem na kumjeruhi mkazi mmoja wakati wakimsaka
mtuhumiwa wa wizi wa pikipiki.
Aliyepigwa na bomu hilo ni Mwanaharusi Hamis ambaye amelazimika kukatwa kiganja cha mkono wa kulia baada ya kujeruhiwa vibaya.
Mwanaharusi alilipuliwa na bomu hilo Agosti Mosi mwaka huu, saa 3 usiku
akiwa nyumbani kwake na sasa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
No comments:
Post a Comment