MTUHUMIWA wa mauaji ya watu tisa na unyang'anyi wilayani Tarime mkoani Mara,
aliyekuwa akihojiwa Polisi kwa tuhuma zilizokuwa zikimkabili, amefariki
dunia katika Hospitali ya Wilaya wakati akipatiwa matibabu ya ugonjwa
wa pumu. Kamanda wa Polisi Tarime na Rorya, Kamishina Msaidizi Justus
Kamugisha, alisema kuwa mtuhumiwa huyo jina lake halisi ni Charles
Kichune (38) na alifariki usiku wa kuamkia jana wakati akitibiwa ugonjwa
huo hospitalini.
Majina mengine aliyokuwa akiyatumia kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha ni pamoja na Josephat Chacha na Charles Msongo.
"Mwili wa marehemu upo chumba cha maiti
katika Hospitali ya Wilaya ukisubiri kufanyiwa uchunguzi na kuchukuliwa
na ndugu zake,” alisema Kamanda Kamugisha.
Baadhi ya raia waliouawa ni pamoja na
David Yomami, Samuel Matiko, Robert Machumbe, Zakaria Marwa , Juma
Nyaitara, Juma Mwita, Marwa Mwita na Erick Makanya.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda
Kamugisha, Kichune baada ya kukamatwa alikiri Polisi kuhusika katika
mauaji ya watu mbalimbali katika kata za Binagi, Turwa na Kitare katika
vijiji vya Mogabiri, Kenyamanyori, Nkende na Rebu.
Kamanda Kamugisha alisema mtuhumiwa huyo
Kichune alikamatwa Februari 6 mwaka huu mkoani Tanga baada ya Polisi
kufuatilia mtandao wake baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Baada ya kukamatwa, uchunguzi wa Polisi
ulibaini kuwa baada ya mauaji ya watu tisa, mtuhumiwa alikodisha
pikipiki kutoka kijiji cha Kenyamanyori alikokuwa akiishi, hadi Musoma.
Alipofika Musoma, inadaiwa alihifadhi
bunduki aina ya SMG na risasi kadhaa kwa mshirika wake, Marwa Keryoba
maeneo ya Bweri na alipokamatwa alimtaja Keryoba kuwa ndiye anayetunza
silaha hiyo. Februari 7 mwaka huu, Polisi walifuatilia silaha hiyo kwa
Marwa na kumkuta mtuhumiwa, ambapo alitakiwa kujisalimisha lakini
alikaidi na kuanza kurushia risasi askari.
“Marwa aliuawa Februari 7 alfajiri Bweri
Musoma, wakati alipotakiwa kujisalimisha na kukaidi na kuanza
kurushiana risasi na askari," alisema Kamanda Kamugisha. *Mtuhumiwa
mwingine Kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha, kuna mtuhumiwa mwingine sugu
wa mauaji ya watu zaidi ya 10, Senso Magabe ameuawa katika majibishano
na Polisi wiki iliyopita.
Hata hivyo katika majibishano hayo,
wenzake watatu walifanikiwa kutoroka na msako unaendelea wilayani hapa
ambapo wananchi wameombwa kutoa ushirikiano Polisi ili kufanikisha
kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Kamanda Kamugisha alisema tayari watu wanne waliokuwa katika mtandao huo wa ujambazi wamefikishwa mahakamani kwa mashitaka ya unyang'anyi na mauaji.
Watuhumiwa waliofikishwa mahakamani ni
pamoja na Kyoma Manguh, Marwa Mwita , Yohana Mgosi na Chacha Bugichere
ambapo kesi zao zitatajwa Februari 19 mwaka huu.
Jana mamia ya wananchi wilayani Tarime
walifurika kuona mwili wa Kichune maarufu Kenonke ambaye amekuwa tishio
kwa wakazi wa wilaya hiyo. Polisi imetangaza zawadi ya Sh milioni moja
kwa atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamata silaha za moto katika
wilaya za Tarime na Rorya.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment