Watu watatu, akiwamo askari polisi
wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kuzuka mapambano
kati ya polisi na raia katika Kijiji cha Igwati, Tarafa ya Malinyi
Wilaya ya Ulanga, Morogoro.
Diwani wa Kata ya Malinyi, Said Kila aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Leon Chikwita, Andrew Likomoka na Edson Kidunda.
Alisema mmoja wa majeruhi Idelfonce
Malenga (35), hali yake ni mbaya baada ya kupigwa risasi shavuni.
Majeruhi wawili majina yao hayakufahamika mara moja.
Diwani Kila alisema mauaji hayo
yalitokea baada ya kundi la wakulima kuvamia Kituo cha Polisi Malinyi
kushinikiza kuachiwa kwa wenzao watatu waliokuwa wanashikiliwa kwa
tuhuma za kumuua mfugaji mmoja wa kijiji hicho hivi karibuni.
"Baada ya kupata taarifa za kukamatwa
kwa wenzao walifika kituo cha polisi ambako, hawakuwakuta watuhumiwa hao
kwani walikuwa wamehamishiwa kituo kingine," alisema diwani huyo.(P.T)
Alisema katika jitihada za kulinda
kituo, polisi walitoa tahadhari mbalimbali za kuwataka wananchi hao
kutawanyika ikiwamo kupiga mabomu ya machozi, lakini waliendelea kukaidi
amri hiyo na badala yake walizidi kujikusanya na kukivamia na kisha
kukichoma moto pamoja na gari la askari lililokuwapo. Katika shambulizi
hilo, ndipo mauaji hayo yalipotokea.
Chagonja eneo la tukio
Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Jeshi
la Polisi, IGP Said Mwema ametuma timu maalumu ikiongozwa na Kamishna wa
Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja kwenda kuongeza nguvu katika
operesheni ya kuwasaka na kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera
Senso ilisema jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, IGP
Mwema ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususan, Kata ya
Malinyi kuwa watulivu na kuendelea kutoa ushirikiano kwa Polisi wakati
uchunguzi ukiendelea.
Chanzo cha mgogoro
Mgogoro kati ya wafugaji na wakulima
wa Igwati ulianza Desemba 13, mwaka huu wakati kundi la wananchi
lilipomkamata mfugaji huyo na kumpeleka katika ofisi za kijiji.
Ilidaiwa kuwa baada ya kumfikisha,
mtendaji wa kijiji alimfungia mtuhumiwa huyo ofisini kwake na kuanza
kuhoji sababu za wananchi kumkamata jambo ambalo linaelezwa kwamba
liliwakera na kuanza kumshambulia hadi kuikimbia ofisi na kumwacha
mfugaji huyo ambaye alishambuliwa na kuuawa.
Kitendo cha kukamatwa na kupigwa hadi
kuuawa kwa mfugaji huyo kinadaiwa kuwa kilikuwa cha kulipiza kisasi
baada ya wafugaji kuvamia nyumbani kwa Mjumbe wa Kamati ya Mazingira,
Victoria Marietha na kumjeruhi vibaya kisha kufariki dunia katika
Hospitali ya Lugala, Malinyi alikokuwa akipatiwa matibabu.
No comments:
Post a Comment