Sunday, December 29, 2013

HII NI KALI YA KUFUNGA MWAKA: MAHARI YASABABISHA NDOA ISIFUNGWE , WAUMINI NA MCHUNGAJI WAKESHA KANISANI MBEYA

Bwana Harusi Fadhili Mahenge akiwa ndani ya Suti akisubiri kufungishwa ndoa 
Bi Harusi Naomi Ngoje akiwa amejilalia chumbani akisubiri hatima ya Wazazi ndipo ajiandae kwenda kanisani tayari kwa kufunga ndoa na mchumba wake waliodumu kwa miezi saba.
Bwana harusi akiwa na mpambe wake kanisani wakimsubiri bibi Harusi
Askofu Kenani Mpalala akiwa katika picha ya pomaja na Bwana Harusi na mpambe wake muda mfupi baada ya kuwasili kanisani
Askofu Keenan Mpalala wa kanisa la Free Pentecost Church of Tanzania akionesha tangazo la Ndoa
Baadhi ya ndugu wa mwanamke wakiwa katika kikao na kuendelea na msimamo wao kuwa mahali lazima imalize ndipo wamtoe binti yao
Jamaa wameshika vichwa hali haieleweki

Baadhi ya akina mama wakiangalia ratiba ya harusi
Kanisani
Baadhi ya waumini na majirani wakisubiri kanisani



KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Familia moja ya Makunguru  Mtaa wa Ilolo Jijini Mbeya imesababisha sintofahamu dhidi ya Familia nyingine baada ya kumkatalia binti yao kuolewa kwa madai ya waoaji kutokamilisha Mahari waliyokuwa wamepangiwa.

Tukio hilo la aina yake limetokea leo ambapo Bwana harusi aliyefahamika kwa jina la Fadhili Mahenge(28) Mkazi wa Songea aliyekuwa amuoe Naomi Ngoje na harusi yao kufungwa katika kanisa la Free Pentecoste Church Of Tanzania(FPCT) lililopo Makunguru Jijini hapa kushindwa kufungwa baada ya wazazi wa Bibi harusi kuzuia ndoa hiyo hadi Mahari itakapokamilika.

Wakizungumzia tukio hilo Nyumbani kwa Familia ya Bibi Harusi, Mjomba wa Bibi Harusi Dickson Ngoje amesema tatizo la wao kugomea ndoa hiyo ni kutaka waoaji kutimiza masharti waliokuwa wamekubaliana awali ambayo hadi siku ya mwisho familia hiyo haijatekeleza.

Amesema siku ya kwanza waoaji walifika Nyumbani kwa Mzee Ngoje na kujitambulisha ambapo walipangiwa taratibu za mahari kwa mujibu wa Mila kuwa watatakiwa kutoa Blanket 2, Mashuka mawili, Mkaja(200,000), mbuzi 4, Majembe 4, Ng’ombe Jike 2 na Ngo’mbe Dume 1 pamoja na fedha taslimu Shilingi Laki 3.

Amesema baada ya Familia hiyo ya Waoaji ambao ni Ukoo wa Mahenge kupangiwa vitu hivyo waliondoka na kuahidi kurudi siku nyingine kwa ajili kukamilisha vitu walivyopangiwa ambapo walirudi Septemba 11, Mwaka huu wakiongozwa na Mshenga aliyejulikana kwa jina moja la Mzee Katete wakiwa na Blanketi 2, Mashuka mawili pamoja na Fedha shilingi 10,000/= ambazo walizipokea na kuwaambia hawawezi kuzungumza chochote juu ya Ndoa.

Mjomba huyo anaongeza kuwa baada ya wiki mbili familia hiyo ilirudi na kukuta Nyumbani kuna ukoo mzima wakiwa na Shilingi 200,000/= ndipo walipoambiwa walipe kiingilio shilingi 100,000/= ndiyo wanaweza kupokelewa nyumbani jambo ambalo walilitekeleza kisha kulipa fedha walizokuwa nazo kama Mkaja na kuomba wapewe kibali cha kuandikisha ndoa na taratibu za kumalizia vilivyobaki zikiendelea.

Anasema tangu hapo Ndoa ilianza kutangazwa Disemba 8 na kuisha Disemba 22, Mwaka huu baada ya kutangazwa mara tatu huku tangazo likiashiria ndoa kufungwa tarehe 28/12/2013 ambapo wazazi wakiahidi kumalizia Mahari iliyobaki kabla ya siku ya kufunga ndoa.

Akizungumzia kwa kirefu kashishe hiyo, Mjomba huyo anasema baada ya wazazi wa Mwanaume kusisitiza kumaliza kila kitu hadi ifikapo Disemba 23, Mwaka huu na wao walijikusanya na kupanga taratibu za sherehe hususani ya kumwaga binti yao(Send Off) ambayo ilifanyika Disemba 24, Mwaka huu.

Aidha baadhi ya ndugu wameongeza kuwa familia hiyo haioneshi uaminifu wa kumalizia Mahari hiyo kutokana na ahadi zisizotekelezeka walizotoa tangu kipindi cha nyuma na kuongeza kuwa hata kwenye sherehe ya kumwaga binti yao walifika baadhi ya ndugu wakiwa na Zawadi tofauti na taratibu zinavyotaka.

Wamesema kwa mujibu wa taratibu za Sherehe za SendOff upande wa Mwanaume unatakiwa kuleta zawadi ambazo ni  nguo za Bibi Harusi za kuvaa siku ya Ndoa Pamoja n Harusi lakini wao hawakufanya hivyo ingawa walikuwa na Nguo ambazo tayari zilikuwa zimetumika.

Kwa upande wa Mchungaji aliyekuwa anataka kufingisha Ndoa hiyo ambaye pia ni Askofu wa Kanisa hilo, Mchungaji Kenan Mpalala alipoulizwa kuhusu hali hiyo amesema kwa mujibu wa taratibu za Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 8 pingamizi litolewe ndani ya siku 21.

Amesema upande wa Wazazi wa Mwanamke ulishindwa kuwasilisha pingamizi lao kanisani kabla ya Siku 21 badala yake walifika kutoa malalamiko kuhusu kutomaliziwa kwa mahali jambo ambalo alisema yeye kama Mwandikisha Ndoa halimhusu bali pande mbili wanatakiwa kulimaliza kabla ya Ndoa.

Naye Bwana Harusi Mtarajiwa Fadhili Mahenge(28) alipoulizwa kuhusiana na suala hilo huku akiwa tayari Kanisani kwa ajili ya Kufungishwa Ndoa alisema anachosubiri ni hatma ya Wazazi wa Mwanamke kama wanaweza kumwachia Mkewe iliwanachodai awe anamalizia taratibu.

Amesema yeye kama yeye kwa sasa hana fedha zozote za kuweza kumalizia anachodaiwa zaidi ya kuomba busara za wazazi wa Mwanamke kumruhusu Ndoa ifungwe ndipo aweze kulipa Mahari anayodaiwa kwa awamu kutokana na hali yake ya kiuchumi kuwa Mbaya.

Ameenda mbali zaidi kwa kusema kama Wazazi wa Mwanamke wataendelea kuwa na Msimamo huo basi hata yeye ataomba arudishiwe kile alichokitoa awali ili ajipange upya kwa ajili ya ndoa baada ya kukamilisha madai yao.
Chanzo: Mbeya yetu blog

No comments:

Zilizosomwa zaidi