Suala la hatma ya Naibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Zitto Kabwe ndilo lililotawala katika siku ya pili ya kikao
cha Kamati Kuu ya chama hicho na kusababisha mvutano mkali miongoni mwa
wajumbe.
Pamoja na ukweli kuwa kulikuwa na ajenda kadhaa
zilizokuwa zimepangwa kujadiliwa katika kikao hicho cha siku mbili
kilichofanyika Dar es Salaam, suala la Zitto ndilo lililochukua muda
mrefu zaidi kujadiliwa.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho
zilieleza kuwa wajumbe waligawanyika makundi mawili, baadhi
wakipendekeza Zitto avuliwe nafasi yake ya Naibu Katibu Mkuu kwa maelezo
kuwa anakwenda kinyume na taratibu za chama hicho na wengine wakipinga
hatua hiyo kwa maelezo kuwa haina tija.
Mpaka saa moja usiku jana gazeti hili likienda
mitamboni, kikao hicho kilikuwa bado kikiendelea na suala hilo
lililokuwa chini ya ajenda ya hali ya siasa nchini.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa chama
hicho, Benson Kigaila aliahidi kuwa taarifa rasmi ya kikao hicho
ingetolewa baadaye na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Tuhuma za Zitto
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
mwanzoni mwa Novemba mwaka huu aliingia katika malumbano na Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho, akituhumiwa
na Lema kuwa anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho
kutoka mashirika mbalimbali nchini.
Pia, aliingia katika malumbano na chama chake
baada ya kutumia kofia yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC), kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake
hazikaguliwi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kauli ambayo jana Kigaila aliitolea ufafanuzi na
kueleza kuwa Chadema kimekaguliwa na hesabu zake tayari zipo kwa Msajili
wa Vyama vya Siasa.
Hekaheka za jana
Mvutano wa jana ulianza baada ya Mbowe kufungua kikao hicho saa 4:00 asubuhi.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa
baadhi ya wajumbe, wakiwamo wabunge, walitaka Zitto avuliwe nafasi
aliyonayo na kuwa mwanachama wa kawaida, huku wengine wakipinga hatua
hiyo kwa maelezo kuwa Zitto hakuwepo katika kikao hicho na kwamba
alipaswa kusikilizwa.
Yaliyojadiliwa
Ajenda za jana
Zitto atinga usiku
“Baada ya hali kuwa hivyo, Mbowe alipendekeza kuwa Zitto
asijadiliwe kwa kuwa hakuwepo katika kikao hicho,” kilieleza chanzo cha
habari hizo.
Zitto alikuwa katika safari ya kikazi huko Sudan Kusini akiwa amefuatana na wajumbe wa PAC.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Zitto alitafutwa na
alituma salamu kwa wajumbe wa kikao hicho akiwaeleza kuwa alikuwa njiani
na kuahidi kuwa angehudhuria mara tu baada ya kuwasili.
“Zitto alituma ujumbe kuwa anakuja katika kikao,
kilikuwa na ajenda nyingi lakini suala lake lilijadiliwa kwa kirefu
sana,” kilieleza chanzo chetu. Licha ya ombi la Mbowe, bado wajumbe
walishinikiza kuendelea kumjadili Zitto hivyo kusbabisha kuchelewa
kujadiliwa kwa ajenda nyingine.
Tangu juzi, siku ya kwanza ya kikao hicho, ulinzi
uliimarishwa nje ya Jengo la Ubungo Plaza na jana walinzi wa chama
hicho, Red Brigade waliwatimua waandishi wa habari waliokaribia eneo
hilo wakisema hayo ni maagizo kutoka kwa uongozi wa juu.
Yaliyojadiliwa
Katika ufafanuzi wake kwa waandishi wa habari jana
jioni, Kigaila alisema kikao hicho kilichoanza juzi, kimejadili mambo
mbalimbali. Alisema juzi kikao hicho kilijadili muhtasari wa vikao
viwili vya dharura vya Kamati Kuu vilivyofanyika hivi karibuni.
“Tumejadili taarifa ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la
Kiembesamaki, Zanzibar unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni...
tunathibitisha kuwa tutashiriki,” alisema.
“Kulikuwa na taarifa ya hesabu za chama
zilizokaguliwa na kupelekwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na taarifa za
fedha za utendaji kuanzia Kamati Kuu iliyopita mpaka Kamati Kuu ya
sasa,” alisema Kigaila.
Huku akionyesha kitabu cha ukaguzi wa fedha mwaka
2010/11 na 2011/12 alisema: “Kamati Kuu imeridhika kuwa chama
kimekaguliwa na hatuna deni kwa msajili.
Ajenda za jana
Alisema kikao cha jana kilijadili ajenda za
uboreshaji wa jengo la makao mkuu pamoja na kupanga upya kurugenzi za
chama hicho pamoja na nguvu kazi ya makao makuu ili kuweza kutekeleza
vizuri majukumu yake.
“Ajenda inayoendelea hivi sasa ni ya uundaji wa programu ya
`Chadema ni Msingi’, ambayo lengo lake ni kukijenga chama katika ngazi
za chini kabisa. Huu ni mpango mkuu wa chama wa `Vuguvugu la Mabadiliko’
(M4C). Ajenda ya mwisho itakuwa ni kujadili hali ya kisiasa nchini.”
Zitto atinga usiku
Zitto alifika katika kikao hicho jana saa 2.24
usiku akiwa na walinzi wanne na habari kutoka ndani zinasema kwamba mara
baada ya kuingia, ajenda ya kumjadili ilirejea. Ilielezwa kwamba
alipewa nafasi ya kujitetea baada ya kusomewa ‘mashtaka’ yaliyokuwa
yakimkabili.
Mwandishi wetu aliyekuwa katika eneo hilo anasema
baada ya kurejeshwa kwa agenda hiyo malumbano makali yalizuka kwani
wajumbe walikuwa wazungumza kwa sauti za juu na jazba kiasi cha kusikika
nje.
No comments:
Post a Comment