Watu 10 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakikabiliwa na shtaka la kumuua kwa kukusudia Mjumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba nchini, Dk Sengondo Mvungi.
Akiwasomea shtaka hilo jana, Wakili wa Serikali,
Aida Kisumo aliwataja washtakiwa hao, Chibago Magozi (32)
mfanyabiashara na mkazi wa Vingunguti Machinjioni, John Mayunga (56)
mfanyabiashara na mkazi wa Kiwalani na Juma Kangungu (29) mkazi wa
Vingunguti.
Wengine ni aliyekuwa mlinzi wa marehemu Dk Mvungi,
Longishu Losingo (29) na Masunga Makenza (40) dereva na mkazi wa
Kitunda, ambaye anatuhumiwa kuwa ni kibaka mzoefu.
Kisumo aliwataja watuhumiwa wengine, Paulo
Mdonondo (30) mkazi wa Tabata Darajani, Mianda Mlewa (40) Mkazi wa
Vingunguti, Zacharia Msese (33) mkazi wa Buguruni, Msungwa Matonya
(30) mkazi wa Vingunguti na Ahmad Kitabu (30) mkazi wa Mwananyamala
wilayani Kinondoni.
Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa washtakiwa hao
kwa pamoja Novemba 3, mwaka huu walifanya kosa hilo la mauaji kinyume
na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kisumo alidai kuwa siku ya tukio, katika eneo la
Msakuzi Kiswegere lililopo eneo la Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao
kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dk Sengondo Mvungi.
Baada ya washtakiwa hao kusomewa shtaka hilo,
Hakimu Sundi Fimbo aliwataka wasijibu kitu chochote kwa sababu Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu haina uwezo wa kulisikiliza shtaka hilo hadi
Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kwa kuwa shtaka hilo halina dhamana na upelelezi
bado haujakamilika, washtakiwa walipelekwa rumande hadi Desemba 5, mwaka
huu itakapotajwa.
Washtakiwa hao waliofikishwa mahakamani hapo
asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi na baada ya kesi, waliondoka
kwa kutumia gari aina ya Land Cruiser KX 06 EFD ambalo lilikuwa
likisindikizwa na gari aina ya Noah namba T 539CCB.
No comments:
Post a Comment