Wednesday, September 11, 2013

KIWETE: MNAONIBEZA MTAUMBUKA 2015

Rais Jakaya Kikwete akiweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Kijiji cha Katunguru/Nyamtelela wilayani Sengerema, mkoani Mwanza juzi.
Rais Jakaya Kikwete amesema wale wote wanaombeza kuhusu utendaji wake, wataona aibu atakapomaliza muhula wake 2015 huku akiwananga baadhi ya wanaCCM kwa kushindwa kuyaelezea mafanikio ya Serikali chini ya chama hicho.
 
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika mikoa ya Mwanza na Geita unaofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC), Rais Kikwete alisema: “Wakati wa kampeni nilibezwa sana, lakini sasa ninawaomba walionibeza kufika vijijini na kuangalia ukamilishaji wa ahadi zangu.
“Nataka waje waone, kwa sasa ninakamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote ili kufikia lengo la Watanzania asilimi 30 kufikiwa na nishati hiyo. Hadi 2015 umeme utakuwa umesambaa nchi nzima.
“Serikali yangu itavunja rekodi ya kusambaza umeme katika vijiji vingi nchini…Tumejenga mtandao wa barabara kwa sasa, hali yetu ya barabara ni bora Afrika Mashariki, tuliahidi meli Bukoba naomba niwaeleze kuwa zinakuja, tena siyo moja ni meli mbili.
“La umeme leo nazindua nataka kuwaeleza walionibeza waje waone sasa ahadi zangu...hayo yote niliyasema kwenye ahadi zangu 2010,” alieleza Kikwete huku akishangiliwa na wananchi.
Mradi huo umegharimu Dola za Marekani 15.54 milioni sawa na Sh24.87 bilioni kwa Mwanza na Geita pekee, fedha ambazo ni asilimia 25 ya Dola za Marekani 62.6 milioni sawa na Sh103.24 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 225 ya upanuzi wa njia za kusambazia umeme katika mikoa kumi nchini.
Rais Kikwete alisema Serikali inajipanga kusambaza umeme na kufikiwa vijiji vyote na kubainisha kuwa mpango huo unakwenda sambamba na uanzishaji wa vyanzo vya umeme ili viweze kuzalisha megawati 3,000 ifikapo 2015 na kwamba ziada itauzwa nje ya nchi.
Septemba 2 mwaka huu, Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ilitangaza kuanza kwa awamu ya pili ya usambazaji wa umeme vijijini, mpango ambao utagharimu Sh881 bilioni na kukamilika Juni 2015.
Katika utekelezaji wa mradi huo, huduma za jamii zitakazopewa kipaumbele katika kuunganishiwa umeme ni shule, zahanati, misikiti, makanisa na visima vya maji.
Mpango huo unatarajiwa kuinufaisha mikoa 24 ya Tanzania Bara, huku wateja 250,000 wa awali wakiunganishwa pamoja na kuhusisha kazi ya usambazaji umeme kwenye makao makuu ya wilaya 13 zisizokuwa na umeme.
Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Ami Mpungwe alisema tayari mikoa 14 imepata makandarasi na ujenzi wa vituo sita vya usambazaji umeme, wakati mchakato wa kuwapata wajenzi katika mikoa 13 iliyokosa wakandarasi awali, unaendelea.
Awananga viongozi wa CCM
Rais Kikwete amewananga baadhi ya viongozi wa chama chake na kusema kuwa ni dhaifu katika uongozi kwani wameshindwa kueleza mafanikio ya Serikali chini ya CCM.
“Baadhi ya viongozi wa CCM pamoja na wanachama wamezubaa kiasi cha kushindwa kuzungumzia mafanikio ya Serikali inayoundwa na CCM, lakini wamekuwa mahodari wa kujadili wanapobezwa na wapinzani.
“Tatizo lenu CCM mmezubaa, huo ndiyo udhaifu wenu mkubwa, kupata maji ya bomba ni hatua kubwa na maendeleo, lakini viongozi wa CCM nyie mmezubaa na ni dhaifu, hamuwezi kueleza mafanikio haya, lazima niliseme hili na ujumbe uwafikie,” alieleza na kuongeza.
“Kwa nini mnasubiri mimi nifike hapa ndipo mje kwenye miradi kama hii, mimi nikija huku siji nikiwa nimebeba miradi hii mgongoni, kwa nini mmekuwa dhaifu wa kuyasema haya na badala yake mmekuwa hodari wa kushupalia dosari zinazosemwa na wapinzani na kuacha mazuri haya?” alisema Kikwete. 

Alisema Tanzania ni nchi kubwa kuliko nchi zingine za Afrika Mashariki, lakini ina mtandao mkubwa wa barabara kuliko nchi kama Kenya, lakini akawalaumu watu wanaoisifia nchi hiyo jirani na kubeza mafanikio ya Serikali yake.
Azungumzia Elimu
Wakati huohuo, Rais Kikwete amewaagiza wakuu wa mikoa kuhakikisha kila sekondari ya kata inakuwa na maabara zenye vifaa viliyokamilika na kwamba atakayeshindwa kufanya hivyo atamwajibisha.
Alisema vijana lazima wasome katika shule zenye vifaa na kusisitiza kuwa, kwa sasa Serikali imekamilisha mpango wa kusambaza walimu ili kukabiliana na uhaba uliopo. 

Rais Kikwete alisema kwa sasa Serikali inajiandaa kukamilisha mpango wa Tehama kwa shule zote nchini kutokana na kuwapo kwa mtandao wa mawasiliano kupitia mkongo wa taifa.
Mwananchi 

No comments:

Zilizosomwa zaidi