Hatua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
kushindwa kufika mkoani Kagera kukagua tuhuma za ufisadi wa miradi
zinazomkabili Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, imezua hofu
kubwa kwa wananchi
Mkaguzi huyo aliagizwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Rais Jakaya Kikwete, kupitia Kamati Kuu ya chama hicho, kukagua miradi
hiyo ili kukata mzizi wa mgogoro unaofukuta.
Kamati Kuu ilitoa agizo hilo Agosti 27 mwaka huu, na kumtaka CAG
kuanza ukaguzi wiki moja baadaye lakini hadi leo zikiwa zimepita siku
14, ukaguzi huo haujaanza.
Wakizungumza mjini Bukoba, baadhi
ya madiwani wa CCM walisema kuwa hatua hiyo inazua hofu kubwa kutokana
na kuwapo kwa mbinu chafu za baadhi ya watendaji wa manispaa hiyo kutaka
kuficha nyaraka.
Madiwani hao walioomba kuhifadhiwa majina yao, walidai kuwa siku
chache baada ya Kamati Kuu kutoa uamzui huo, baadhi ya watendaji wa
maispaa hiyo walikesha ofisini kwa siku mbili, jambo lililotafsiriwa
kama mkakati wa kubadili nyaraka kabla CAG hajaanza ukaguzi.
“Haya mambo yanachekesha, maana wananchi wamechanganyikiwa hapa,
ilikuja kamati ya waziri mkuu chini ya Abbas Kandoro, ikachunguza lakini
ripoti yake hadi leo haikuletwa.
“Sasa kuchelewa huku kwa CAG tunaanza kupata shaka kuwa ni mambo
yaleyale ya CCM kufunika kombe ili kumlinda meya, maana siku 14
zimepita, kwani huyo mkaguzi anatoka wapi kama hafiki?” walihoji.
Madiwani hao walionya kuwa hali itakuwa mbaya kama CCM itaendelea
kufumbia macho ufisadi huo kwani wapinzani wanazidi kuungwa mkono.
Alipoulizwa Mkuu wa Mkoa huo, Fabian Massawe, kuhusu ujio huo wa CAG,
alisema yuko kwenye operesheni, hivyo kuelekeza atafutwe Mkuu wa Wilaya,
Zipola Pangani.
Pangani alikiri kuwa CAG hajaanza kazi lakini akasisitiza kuwa atafika
wakati wowote kwani hayo ni maagizo, hivyo lazima afanye ukaguzi.
Katika kumaliza mgogoro wa umeya mjini Bukoba, Kamati Kuu ya CCM
alitengua uamuzi wa kuwafukuza madiwani wanane wa manispaa hiyo, ambapo
chama kilidai kuwa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kagera iliyokuwa
imewafukuza ilikiuka Katiba.
Kamati hiyo ilimwagiza CAG kwenda mjini Bukoba kukagua tuhuma hizo
dhidi ya meya, kisha ripoti hiyo kuwasilishwa kwenye baraza la madiwani
ili hatua zaidi zichukuliwe kama ikithibitika alifanya ufisadi.
Katika kikao hicho, Rais Jakaya Kikwete alikiri timu iliyoundwa na
waziri mkuu kuchunguza mgogoro huo kuwa ilibaini mianya ya ufisadi
katika manispaa hiyo.
“Rais alisema hawezi kumfukuza meya kwa vile mamlaka hayo yako kwa
madiwani waliomchagua, hivyo aliagiza CAG aende Bukoba kuchunguza tuhuma
hizo halafu ripoti iwasilishwe kwenye baraza la madiwani hatua
zichukuliwe,” kilisema chanzo chetu.
Baada ya ukaguzi huo madiwani wanaweza kufanya lolote wanalotaka. Kama ni kumfukuza meya au la, wataamua wao.
Madiwani hao wanane na kata zao kwenye mabano ni Richard Gaspar
(Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye
pia ni Naibu Meya (Buhembe) na Yusuf Ngaiza.
Wengine ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa
(Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na
Dauda Karumuna (Ijuganyondo).
Vile vile, Rais Kikwete aliwataka meya na mbunge wafanye jitihada za
kupatana na kufanya kazi pamoja kama ilivyokuwa zamani; hata wakitaka
kutumia viongozi wa dini au wa kisiasa.
Rais pia aliagiza viwanja 800 vilivyokuwa na mgogoro, warudishiwe
wananchi waliokuwa wanavimiliki na wasitozwe hata senti tano.
Madiwani hao wamekuwa wanamlalamikia meya kuwa ameiingiza manispaa katika ufisadi kwenye miradi kadhaa.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh
bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) ambao haukufuata
taratibu na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha
malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata
utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani.
Vilevile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90 lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka.
Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134 za ujenzi wa kituo cha mabasi.
No comments:
Post a Comment