Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amezungumza kwa simu na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na kumpa pole na
kutaka kujua jinsi gani Tanzania inaweza kusaidia kufuatia shambulio la
kigaidi kwenye Kituo cha Biashara cha Westgate katika eneo la Westlands,
Nairobi, ambako watu 59 wameuawa na wengine 175 wamejeruhiwa.
Rais
Kikwete alimpigia simu Rais Kenyatta jioni ya Jumamosi, Septemba 21,
2013, kutokea mjini New York, Marekani, mara baada ya kuwasili mjini
humo akitokea Toronto, Canada, ambako alifanya ziara ya kikazi ya siku
tatu.
Katika
mazungumzo kati ya viongozi hao, Rais Kikwete amemweleza Rais Kenyatta
mshtuko na hasira yake kutokana na taarifa za kusikitisha za shambulio
hilo la kigaidi lililofanywa asubuhi ya jana hiyo hiyo.
Rais
Kikwete amefuatilia mazungumzo hayo kwa salamu rasmi za rambirambi
ambazo Rais Kikwete amemtumia Rais Kenyatta akielezea masikitiko na
hasira yake kufuatia mauaji hayo ya watu wasiokuwa na hatia akitaka
kujua jinsi Tanzania inaweza kusaidia juhudi za Serikali ya Kenya katika
kukabiliana na madhara ya tukio hilo na balaa la ugaidi kwa jumla.
Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Kikwete amemweleza Rais Kenyatta: “Nimekupigia
simu mapema leo kuelezea mshtuko na hasira yangu baada ya kusikia
habari za kusitikisha za shambulio la kigaidi lililotokea asubuhi ya
leo, Jumamosi, Septemba 21, 2013, kwenye Kituo cha Biashara cha Westgate
katika eneo la Westlands na kusababisha vifo vya watu 59 na mamia ya
majeruhi.”
Katika salamu zake hizo za rambirambi RaisKikwete amesema: “Kwa
niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa hakika,
kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kutuma salamu za dhati ya moyo wangu
kwako wewe, kwa Serikali ya Jamhuri ya Kenya na kwa familia zote
zilizopotelewa na wapendwa wao katika shambulio hili. Sala zetu na pole
zetu nyingi ziko pamoja na wale wote ambao wameathiriwa na shambulio
hili la kutisha. Aidha, tunawatakia walioumia kasi ya kupona.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Shambulio
hili linalenga kuitisha Serikali na Wananchi hodari wa Kenya na
kudhoofisha nia yao ya kutimiza wajibu wao wa kihistoria wa kuunga mkono
jitihada za kuleta amani katika nchi jirani na yenye matatizo ya
Somalia.”
“Kwa
maana hiyo, shambulio hilo la woga na lisilo na huruma kabisa dhidi ya
watu wasiokuwa na hatia, lazima lilaaniwe na kushutumiwa vikali na
wapenda amani wote”.
“Tuna
hakika kuwa chini ya uongozi wako imara, Serikali ya Kenya itahakikisha
kuwa wote waliohusika kufanya kitendo hiki wanasakwa nakufikishwa mbele
ya vyombo vya sheria kama ambavyo Serikali imepata kufanya huko nyuma,” Rais Kikwete amesisitiza na kuongeza:
“Serikali
na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanasimama bega kwa bega
na kaka na dada zao wa Kenya katika kipindi hiki kigumu. Aidha,
Serikali ya Tanzania inapenda kuihakikishia Serikali ya Kenya itaendelea
kuiunga mkono na kushirikiana nayo katika kupambana na balaa la ugaidi
katika sura zake zote.”
No comments:
Post a Comment