Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemwondolea Meneja Uendelezaji Biashara wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Theophil Makunga, hati ya kumkamatwa.
Hakimu Mkazi, Warialwande Lema, juzi alitoa amri
ya kumkamata Makunga na kumfikisha mahakamani, baada ya kuchelewa kufika
kortini kuhudhuria kesi ya kuchapisha makala inayodaiwa kuwa ya
uchochezi inayomkabili yeye na wenzake wawili.
Hata hivyo, Mahakama hiyo jana ilimwondelea hati
hiyo baada ya kujisalimisha mwenyewe na kujieleza sababu za kutowahi
wakati kesi hiyo ikitajwa.
Makunga alidai kuwa hakudhamiria kutofika mahakamani, bali alichelewa kwenye foleni.
Akizungumzia hatua ya kumwondolea hati ya kumkamata, Makunga alisema amefurahi na anashukuru kwa uamuzi huo.
Kesi hiyo ilitajwa juzi, lakini hadi wakati mahakama inaanza, Makunga alikuwa hajafika mahakamani.
Wakili wake, Frank Mwalongo alidai kuwa mteja wake alikuwa njiani na kwamba, alikuwa amekwama kwenye foleni.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Lilian Itemba
aliomba Mahakama itoe amri ya kumkamata mshtakiwa, ombi ambalo Hakimu
Lema alilikubali.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 20, mwaka huu,
itakapotajwa tena mahakamani hapo. Makunga ni mshtakiwa wa tatu
aliunganishwa kutokana na gazeti la Tanzania Daima, kuchapishwa kwenye
kiwanda cha MCL.
No comments:
Post a Comment