Serikali ya Tanzania imesema itahakikisha
inaendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kwa Watanzania na raia
wa kigeni waliopo na wanaoendelea kutembelea hapa nchini kwa ajili ya
utekelezaji wa shughuli mbalimbali za binafsi na kimaendeleo ili watu
wote waweze kutekeleza majukumu yao na kuishi kwa amani na usalama
nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi alisema hayo jana wakati akizungumza katika kikao baina yake na
Ujumbe wa Wawakilishi wa nchi za Umoja wa Ulaya na mabalozi wa nchi hizo
hapa nchini kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa wizara hiyo.
Taarifa ya wizara ilisema Nchimbi alisema kwa sasa
Serikali kupitia polisi imejiwekea mikakati mbalimbali ya kukabiliana
na vitendo vya uhalifu katika Jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa
ujumla.
‘‘ Polisi tayari imeanzisha dawati maalumu
litakalowahudumia raia wa kigeni ili kuwawezesha kufungua kesi zao kwa
urahisi, kuwapo kwa wepesi wa majadiliano na ziweze kushughulikiwa kwa
haraka na hatimaye kupatiwa ufumbuzi”, alifafanua Waziri Nchimbi.
Waziri Nchimbi alisema pia katika kusimamia suala
la ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa sasa wizara yake itafanya
ukaguzi wa kampuni binafsi za ulinzi ili kuangalia na kujiridhisha kama
zinakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.
Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe wa Wawakilishi
wa Nchi za Umoja wa Ulaya hapa nchini, Balozi Filberto Cerani Sebregondi
alisema umoja huo utaendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi ambapo pia aliishukuru kwa jitihada inayoendelea kuchukua
kuhakikisha ulinzi na usalama kwa wageni na raia wa Tanzania unaimarika.
Kwa upande wao mabalozi waliohudhuria kikao hicho
waliitaka Serikali na Watanzania kuhakikisha usalama unadumishwa ili
kutoathiri taswira ya Tanzania kimataifa na hivyo kuhatarisha uwezekaji
na utalii.
Walisema Umoja huo una imani na Serikali kwamba
itaimarisha zaidi masuala ya ulinzi na kuhakikisha raia wote wanalindwa
kwa haki.
chanzo: Mwananchi
chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment