Wednesday, May 22, 2013

HII NI KWA AJILI YA "CCM" NA "CHADEMA"

 
 
 
 
 
MWENENDO wa Bunge la Bajeti linaloendelea mjini hapa, umebaini kuwa vita ya maneno, fitna kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), sasa imehamia bungeni, Tanzania Daima Jumatano limebaini.

Moto wa vita hiyo kati ya vyama hivyo hasimu, umekolezwa zaidi baada ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete kufanya mkutano wa kimkakati na wabunge wa chama chake mjini hapa.

Duru za siasa kutoka ndani ya kikao hicho cha wabunge na rais, zilieleza kuwa Rais Kikwete aliwataka wabunge hao wa CCM wajipange kukabiliana na hoja za CHADEMA ambazo katika siku za hivi karibuni zimeonekana kulitikisa Bunge kiasi cha kiti cha spika kuamua kutumia kanuni kandamizi kuzizima.

Wabunge wa CCM bila kujali uzito wa hoja, wameamua kukabiliana na hoja zozote za wabunge wa CHADEMA hata kama zina maslahi kwa taifa.

Tayari CHADEMA kimeeleza kubaini mbinu hizo, kikidai kuwa hata kitendo cha Spika Anne Makinda kukatisha hotuba ya msemaji wao katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika alisema kuwa hatua hiyo ndiyo iliwafanya wasikubali kubadili hotuba yao hiyo kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa 14 kama ilivyotakiwa na spika kwani ni kinyume na kanuni ya 63 (2).


Kanuni hiyo inasema kuwa mbunge yeyote anayekuwa akisema bungeni hatachukuliwa anasema uongo iwapo atafanya rejea ya habari.

“Hivyo kambi kunukuu ripoti za Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri (TEF), ile ya Kamati ya Waziri Emmanuel Nchimbi, makala ya Ndimara Tegambwage, Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari Ulimwenguni (CPJ) na Tume ya Haki za Binadamu haijavunja kanuni,” alisema.

Mnyika alifafanua kuwa CCM inafanya siasa bungeni kwa kuitumia vibaya kanuni ya 64 (1) (c) inayozuia mambo yanayosubiri uamuzi wa mahakama na kwamba ndiyo maana aliwahi kukata rufaa kuhusu jambo hilo.

“Kwa hiyo tulibaini mkakati wao huo wa kutaka kuzima hoja yetu iliyokuwa ikizungumzia vitendo vya utekaji na utesaji wa wanahabari ili kudhibiti hoja zenye ukweli,” alisema Mnyika.

Hata hivyo, kwa jinsi mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari ulivyoendeshwa na Spika Makinda, imeonesha wazi kuwa kuna upendeleo kwa wabunge wa CCM hasa wanapochangia kujibu hoja za CHADEMA.

Mathalani Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kigoma, Sabrena Sungura (CHADEMA) jana alizuiliwa na spika kunukuu makala ya mwandishi nguli nchini Tegambwage iliyochapishwa katika gazeri la Tanzania Daima ikiwataja waandishi wa habari waliowahi kupata vitisho, kuumizwa na kuuawa.

Licha ya kanuni za Bunge kumpa fursa ya kufanya hivyo, lakini katika hali ya kushangaza spika alimtaka asiendelee kuzungumza suala hilo kwa madai kuwa ni uchochezi kwa kuwa matukio mengine kesi zao ziko mahakamani.

Lakini muda mfupi baadaye, Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati wakati akichangia alidai kuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), aliwachochea vijana mjini humo wafanye vurugu na hivyo vijana hao zaidi ya 50 kufikishwa mahakamani.

Licha ya Kabati kuzungumza suala hilo kwa makusudi wakati akijua liko mahakamani, si spika wala Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyeshtuka kumzuia kuendelea kufanya hivyo, badala yake wabunge wa CCM walizidi kumpigia makofi.

Hata Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba katika mchango wake aliwashambulia wabunge wa CHADEMA hususani Mnadhimu wao Mkuu, Tundu Lissu akidai kuwa wanahitaji kupelekwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kujifunza uzalendo waache kuzungumza kauli za uchochezi bungeni.

Pamoja na kwamba Komba alidanganya Bunge kwa vile Lissu amepitia JKT mwaka mmoja kupitia Oparesheni Programu ya Chama mwaka 1989 hadi 1990, Spika wa Bunge naye aliunga mkono akisema apelekwe huko mwaka mmoja.

Wabunge wengi wa CCM waliochangia hotuba hiyo, walijaribu kuvishambulia vyombo vya habari wakidai vinawaandika sana CHADEMA kuliko wabunge wengine.

Katika kile kinachoonesha kuwa wabunge wa CCM wanaumizwa na mwenendo wa vyombo hivyo kuwapa nafasi kubwa viongozi wa upinzani kuliko wale wa serikali, Mbunge wa Viti Maalumu, Tuahida Nyimbo (CCM) alishauri uwekwe utaratibu wa habari kutangazwa kwa kufuata itifaki.

Mbunge huyo alisema inashangaza kuona taarifa za habari zinaanza kuwaonesha watu wengine kama wabunge wanaofanya vurugu bungeni na ile ya rais anayeelezea maendeleo inawekwa mbali.

Katika kuhaha huko kujinusuru bungeni, CCM katika kikao chake baina ya wabunge na Rais Kikwete, iliwanyoshea vidole wabunge wake watatu ikipinga hatua yao ya kuikosoa serikali kwa mtindo unaowapa nguvu CHADEMA.

Wabunge hao ni Kangi Lugola (Mwibara), Deo Filikunjombe (Ludewa) na Luhaga Mpina (Kisesa) ambao hata hivyo wote wameapa kuendelea na msimamo wao wa kuikosoa serikali na kupinga ufisadi pale watakapobaini upungufu.

Mmoja wa wabunge hao ambae aliomba kuhifadhiwa jina, aliliambia gazeti hili jana kuwa wanachokifanya ni kukemea ufisadi serikalini na kupinga uzembe kwa baadhi ya mawaziri.

“Mafisadi wanatishika na msimamo wetu, sisi hatuna mpango wa kukibomoa chama ila tunakisaidia kwa kuwasema hao wanaojificha humo na kujifanya wakereketwa wakuu,” alisema.

Wabunge hao watatu pamoja na wengine baadhi wa chama hicho wamekuwa mwiba mkali kwa mawaziri kutokana na kuzipinga bajeti zao.

Mfano Lugola hivi karibuni aliwashambulia wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), akitishia kuwataja baadhi yao na watendaji wanojihusisha na rushwa pamoja na biashara ya dawa za kulevya.

Filikunjombe na Mpina nao wamekuwa na msimamo wa kukataa kuunga mkono bajeti za serikali zinazokuwa hazina maslahi kwa wananchi.

Katika kikao hicho cha CCM, Kikwete aliwataka wabunge kuendelea kuisimamia serikali pale inapobidi, lakini akawasihi wafanye hivyo kwa staha bila kutumia maneno makali akitumia mfano “serikali imevaa miwani ya mbao” kauli aliyowahi kuitumia Filikunjombe hivi karibu akimaanisha si sikivu.

Chanzo chetu ndani ya kikao hicho kilieleza kuwa Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba ndiye alikuwa mwiba mkali kwa kuwashambulia wabunge hao, akidai wamekuwa na tabia isiyokoma.

Nkumba ambaye si mara yake ya kwanza kuwashambulia wenzake hao, alipendekeza kuwa kama wanataka ni heri wakahamia CHADEMA kuliko kuendelea kuivua nguo Serikali ya CCM.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Zilizosomwa zaidi