Tuesday, April 2, 2013

RUFAA YA ZOMBE KUSIKILIZWA APRIL 22.

Rufaa ya Jamhuri dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na askari wenzake wanane, sasa imepangwa kusikilizwa mwezi huu.

Awali rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa na Mahakama ya Rufani Desemba 11, 2012, lakini ilikwama kutokana na kuugua kwa Jaji Semistocles Kaijage ambaye alikuwa ni mmoja katika jopo la majaji waliopangwa kuisikiliza. Majaji wengine katika jopo hilo walikuwa ni, Jaji Nathalia Kimaro na Jaji Catherine Oriyo.
 
Hata hivyo kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya mahakama hiyo vya mwezi April, sasa rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa Aprili 22 na 23, 2013, kuanzia saa 3:00 asubuhi. Ratiba hiyo pia inaonyesha kuwa rufaa hiyo itasikilizwa na jopo la majaji watatu tofauti na wale wa kwanza. Majaji hao ni Edward Rutajangwa,  Salum Mbarouk na Bernard Luanda.
Zombe na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva wa teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam.
 Agosti 17, 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam  iliwaachia huru washtakiwa wote ikisema kuwa baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za mawakili wa pande zote imeridhika kuwa washtakiwa hawakuwa na hatia.

No comments:

Zilizosomwa zaidi