KAMBI
zinazosigana ndani ya CCM zinaonekana kuchuana vikali katika uchaguzi
wa ngazi ya wilaya ya chama hicho tawala, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa
2015, huku Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akionekana kupata
mafanikio, ikilinganishwa na mahasimu wake, Benard Membe na Samuel
Sitta.
Kama ilivyo kwa Lowassa, Sitta ambaye ni Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Membe ambaye ni Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wamekuwa wakitajwa kuwa kwenye harakati
za kuusaka urais, hivyo uchaguzi wa ndani wa CCM ni fursa ya kupanga
safu za kufanikisha mikakati hiyo.
Lowassa binafsi tayari amepita
katika kinyang’anyiro hicho kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia Wilaya ya Monduli. Jana
mbunge huyo wa Monduli alitoa kauli kali akisema kuwa wapo watu
wanaovuruga CCM katika Wilaya ya Monduli na kwamba tayari amewabaini,
hivyo kuahidi kwamba watashughulikiwa kisiasa.
''Yako maneno ya
ovyoovyo yamekuwa yakipikwa ya kuwaandama viongozi wa CCM Monduli,
yanasemwa na wakubwa fulani, yanapikwa na watu fulani wa Monduli,
tunawajua. Nataka kuwaambia tumewajua na nawaambia hawatuwezi,''
alitamba Lowassa.
Lowassa alisema ushindi alioupata umedhihirisha kuwa ana misuli ya kisiasa na kwamba wakazi wa Monduli ndiyo msuli huo.
''Kuna
mzee rafiki yangu aliniambia kuwa katika kazi za siasa angalia
‘grassroots’. Watu wanakuwa ndiyo msuli wako kisiasa na mimi watu wa
Monduli ndiyo msuli wangu,'' alisema.
Aliendelea ''Wananchi wa
Monduli mmenithibitishia hilo na nawashukuru sana kutoka kwenye ‘sakafu’
ya moyo wangu, jibu la thibitisho hilo kwangu ni utumishi uliotukuka.''
Kwa
upande wake, Membe anasubiri kuparurana na vigogo wenzake katika kundi
la kifo la ujumbe huo katika uchaguzi wa ngazi ya Taifa, wakati Sitta
tayari ni mjumbe wa NEC akiwakilisha wabunge wa CCM katika chombo hicho
kikubwa cha uamuzi ndani ya chama hicho.
Matokeo katika maeneo
kulikomalizika uchaguzi wa ngazi ya wilaya yanaonyesha kuwa Lowassa
amefanikiwa kupanga safu yake vizuri zaidi, ikilinganishwa na wenzake
hao.
Membe anaonekana kufuata kwa karibu na Sitta ni kama
anashika mkia kwa kuwa na wafuasi wachache waliofanikiwa kuchaguliwa.
Hata hivyo, chaguzi katika baadhi ya mikoa bado zinaendelea, huku
uchaguzi wa ngazi za mikoa na taifa ukisubiriwa kwa hamu.
Manyara na Arusha Kundi
la Lowassa lilizidi kupata nguvu baada ya mfuasi wake mpya ambaye ni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk Mary
Nagu kumbwaga Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Sumaye naye
anatajwa kuwa miongoni mwa ‘wanaoutaka’ urais na kuanguka kwake katika
uchaguzi wa Hanang, kunatia doa kubwa harakati zake hizo.
Katika
uchaguzi uliofanyika jana kwenye Wilaya ya Arusha Mjini, Lowassa
ameibuka kidedea kwa wapambe wake kadhaa kuchaguliwa, huku mwenyekiti wa
zamani wa CCM wa Wilaya hiyo, Jubilate Kileo akiangushwa na Dk Wilfred
Ole Soilel.
Katika kinyang’anyiro cha mjumbe wa Nec, Godrey
Mwalusamba alishinda na kuwaangusha vibaya wapinzani wake ambao ni Loota
Laiser na Dk Harold Adamson.Kuchaguliwa kwa Dk Ole Soilel anayehusishwa
na kambi la Lowassa kuliibua simanzi kwa kambi nyingine ambapo katika
hali isiyo ya kawaida, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na Katibu
wa CCM Arusha, Mary Chatanda walionekana kuwa wanyonge muda wote.
Mwanza na Dodoma Mkoani
Mwanza, kambi za Lowassa na Membe zinatajwa kuchuana vikali huku kukiwa
na sintofahamu kwamba mgombea wa nafasi ya mweyekiti wa mkoa huo,
Anthony Diallo yuko upande upi.
Diallo ambaye alianguka katika
uchaguzi wa ubunge Oktoba 2010, anaonekana kurejea kwa nguvu mpya, kwani
tayari baadhi ya wale wanaotajwa kuwa wafuasi wake wametwaa nafasi
muhimu katika uchaguzi wa wilaya.
Hata hivyo, kada huyo wa siku
nyingi wa CCM ambaye anamaliza muda wake wa ujumbe wa NEC akiuwakilisha
Mkoa wa Mwanza, anakabiliwa na kibarua kigumu Oktoba 13, mwaka huu,
atakapopambana na mweyekiti anayetetea nafasi yake Clement Mabina,
Zebedayo Athumani na Joseph Langula Yared.
Kwa sasa kuna taarifa
kwamba Diallo anamuunga mkono Membe hivyo ushindi wa wafuasi wake katika
Wilaya za Nyamagana, Ukerewe, Misungwi na Sengerema unaweza kuinufaisha
kambi hiyo.
Mabina ambaye anatajwa kuwa mshirika wa Lowassa, katika matokeo ya awali, kambi yake inaonekana kutokufanya vizuri.
Ushindi
muhimu katika Wilaya ya Nyamagana ulikuwa ni wa nafasi ya Mwenyekiti
iliyonyakuliwa na msadizi wa siku nyingi wa Diallo, Raphael Shilatu,
ambaye aliwabwaga Mashaka Kaguna aliyetajwa kuwa mfuasi wa Lowassa na
Yahya Nyaonge anayetajwa kuwa mfuasi wa Sitta.
Hata hivyo,
ushindi huo unatajwa kutiwa doa na mmoja wa wafuasi wa Lowassa ambaye ni
mbunge wa zamani wa Nyamagana, Lawrence Masha ambaye alikuwa mjumbe wa
NEC.
Wilayani Ukerewe kambi ya Membe inatajwa kushinda kiti cha
Uenyekiti kupitia Ally Mabile na katika Wilaya ya Busega kambi ya Sitta
inatajwa kutwaa ujumbe wa NEC kupitia kwa mbunge wa zamani wa Busega, Dk
Raphael Chegeni.
Mkoani Dodoma matokeo ya uchaguzi wa nafasi
mbalimbali yanaonyesha kwamba kambi ya Lowassa imefanya vizuri hasa
katika Wilaya za Dodoma Mjini, Bahi, Kondoa, Chemba na Kongwa.
Hata
hivyo, ngome ya Waziri Mkuu huyo wa zamani imeangukia pua katika Wilaya
ya Chamwino, baada ya wapambe wake kubwagwa na wale wanaotajwa kumuunga
mkono Sitta. Katika Wilaya ya Mpwapwa viongozi waliochaguliwa ni wapya
na hadi sasa haifahamiki wanaunga mkono kambi gani.
Dar, Zanzibar na Moro Visiwani
Zanzibar, Lowassa aliendelea kupeta kutokana na ushindi wa aliyewahi
kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Hamad Yussuf Masauni, ambaye
alishinda nafasi ya ujumbe wa NEC na kumbwaga aliyekuwa Naibu Waziri wa
Habari Utamaduni na Michezo, Mahamoud Thabiti Kombo.
Akitangaza
matokeo ya uchaguzi huo Katibu wa Wilaya ya Mjini, Fatma Juma Shomari
alisema kwamba kati ya wagombea 19 waliokuwa wakiwania nafasi sita za
NEC, Masauni aliibuka mshindi wa pili akitanguliwa na Naibu Katibu Mkuu
wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
Aliyeshinda nafasi ya uenyekiti ni
Juma Faki Chumu na wajumbe wengine wa NEC ni Buruhani Saadati Haji,
Asha Abdalla Juma, Talib Ali Tali Sufiani Khamis Ramadhani na Omar
Jastus Morris.
Hata hivyo, katika Mkoa wa Dar es Salaam, kambi ya
Lowassa ilipata pigo kutokaana na kubwagwa kwa Naibu Waziri wa Kazi na
Ajira, Dk Makongoro Mahanga aliyekuwa akiwania nafasi ya ujumbe wa NEC
kupitia Wilaya ya Ilala.
Kadhalika mkoani Morogoro, kambi hiyo
pia ilipata pigo kutokana na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Amos Makala kubwagwa na Suleiman Ahmed Sadiq katika
uwakilishi wa NEC Wilaya ya Mvomero.
Taarifa kutoka mkoani
Tabora zinasema katika wilya zote za mkoa huo, kambi ya Lowassa
imeshinda kwa kishindo isipokuwa Wilaya ya Urambo ambayo kambi ya Sitta
inadaiwa kuibuka kidedea.
Wasomi wanena Baadhi ya wasomi
nchini, wametofautiana kimtazamo kuhusu chaguzi ndani ya CCM huku
wengine wakisema chama hicho kimeshindwa kuwadhibiti vigogo wanaotajwa
kuwania nafasi ya urais ambao wamefanikiwa kuwaingiza wafuasi wao kwenye
nafasi mbalimbali za uongozi.
Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu
cha Mwalimu Nyerere, Sabun Parit alisema hatma ya chama hicho kuelekea
Uchaguzi Mkuu ujao ni nzuri kutokana na kufanikiwa kuendesha uchaguzi
wake kwa utulivu.
“Mara nyingi tumezoea kuona makundi yakiibuka
wakati wa uchaguzi, lakini safari hii hali ni shwari, hatujasikia
makundi wala malalamiko na hii ni ishara kwamba hiki chama kimekomaa na
hakiwezi kutetereka,” alisema mhadhiri huyo.
Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitilya Mkumbo ambaye pia ni Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chadema alisema jana kuwa CCM imeshindwa kuwadhibiti
vigogo hao ndani ya chama hicho na hivyo wameanza vizuri katika
maandalizi ili kupitishwa na chama hicho kugombea kiti ya urais.
“Kwa
kweli CCM wamejimaliza na wameonekana kuwa hawana jipya, wale waliotaka
kuwavua magamba ndiyo haohao wamepitishwa kwenye uchaguzi pamoja na
wafuasi wao kuwasaidia katika Uchaguzi Mkuu,” alisema Dk Mkumbo.
Naye Mhadhiri wa UDSM, Dk Benson Bana alisema CCM imeonyesha kwamba hakuna kiongozi yeyote mwenye hatimiliki ya chama hicho.
“Kwa namna mambo yalivyoonyeshwa kwenye uchaguzi huo, mtu yeyote anaweza kuingia na kuondoka kwenye chama hicho,” alisema.
Naye Kisena Mabuba ambaye pia ni Mhadhiri katika Chuo cha Mwalimu Nyerere alisema uchaguzi huo umefuta makundi ndani ya CCM.
“Tofauti
na matarajio ya wengi kuwa CCM ingemeguka, mimi ninachokiona hapa kundi
lililobaki na nguvu ni lile la mwenyekiti mwenyewe. Kundi moja
limefutwa kabisa na mengine yameshindwa kupata nguvu za kutosha,”
alisema Mabuba.
Alitaja mbinu zilizotumika kufuta makundi hayo
kuwa ni hatua ya kubadili katiba na kuwaweka pembeni marais wastaafu
pamoja na uteuzi wa makatibu wa chama ngazi ya mikoa na wilaya ambao
walifanya makundi kupoteza nguvu.
Chanzo; gazeti la Mwananchi.
|
No comments:
Post a Comment