Friday, February 14, 2014

SERIKALI YATAFUTA MWEKEZAJI USAFIRI WA TRENI

 
SERIKALI imeruhusu mtu yeyote mwenye uwezo wa kuwekeza katika usafiri wa treni ajitokeze, ili kuuboresha.
 
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, alieleza hayo mjini hapa jana katika kongamano la uwekezaji Kanda ya Ziwa uliokuwa ukijadili mambo mbalimbali yatakayoweza kunyanyua uchumi wa Kanda ya Ziwa kwa kuzingatia sekta sita muhimu.

Moja ya sekta hizo ni ya uchukuzi ambao wawekezaji wa Kanda ya Ziwa walieleza kuwa ili kuweza kunyanyua uchumi na kuvutia wawekezaji ni lazima kuwepo na miundombinu mizuri ambayo ni viwanja vya ndege, treni na barabara.

Akijibu hilo, Tizeba alisema ni kweli kuna changamoto katika miundombinu Kanda ya Ziwa ikiwa ni pamoja na usafiri wa treni ambao ungesaidia katika usafirishaji wa mizigo badala ya kutumia barabara ambazo zina gharama kubwa huku akitolea mfano mtu anaweza kusafirisha kwa sh milioni tatu badala ya milioni moja au 500,000.

Kutokana na hali hiyo, alisema serikali inaruhusu uwekezaji katika njia ya treni kwa mtu kununua mabehewa ya abiria na mizigo na kufanya mazungumzo na wizara tayari kwa kuanza kazi.

Hata hivyo alisema hadi ifikapo mwakani, serikali itakuwa imeshaingiza nchini vichwa vya treni 13, locomotive 50, mabehewa mapya ya abiria 274 na  ya mizigo 990.

Hata hivyo, alisema hadi kufikia Juni kutakuwa na mabehewa mapya 22 ya mizigo na pia mabehewa 1,960 yatapatikana ndani ya miaka miwili ya fedha ijayo.

Akizungumzia kuhusu usafiri wa ndege, alisema atahakikisha anasimamia upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza.

“Sio tu kuurefusha uwanja huo bali hata kutengeneza sehemu ya abiria, tufanye marekebisho sehemu ya michoro, pia uendelezaji wa uwanja wa ndege wa Bukoba na kwamba kwa sasa tani 50 zinatua na kuwepo na uwezo wa kushusha abiria 70 kila siku,” alisema Tizeba.

Kongamano hilo litatilia mkazo uendelezaji wa sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili na utalii, miundombinu, huduma za jamii na nishati, sekta ambazo zina fursa nyingi katika Kanda ya Ziwa.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Zilizosomwa zaidi