Sunday, October 21, 2012

KIONGOZI WA TAASISI YA KIISLAMU ZANZIBAR AJITOKEZA

ADAI ALICHUKULIWA NA POLISI, ALIFUNGWA KITAMBAA USONI, WALIMHOJI WAKAMREJESHA  WALIKOMCHUKUA

KIONGOZI wa Taasisi za Kiislamu Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed aliyepotea kwa siku nne visiwani Zanzbar, ameonekana na kudai alichukuliwa na polisi  na kurejeshwa juzi mahali walipomchukua.

“Naomba watu watulie, wasifanye fujo na wasifanye vurugu za aina yoyote. Hizi ni awamu za kudai haki, lakini wawe na subira kwani hii ni nchi yetu na tunaipenda. Tutaitetea kwa nguvu zote,” alisema kiongozi huyo alipohojiwa na gazeti hili jana.

Hata hivyo, awali Jeshi la Polisi Visiwani Zanzibar kupitia kwa Kamishna wake Mussa Ali Mussa lilikanusha kumshikilia kiongozi huyo wa Uamsho.

Mji wa Zanzibar jana ulianza kurejea katika hali ya kawaida kwa wafanyabiashara kuanza shughuli zao huku magari ya abiria yakiwa yamejaa watu kituo kikubwa cha magari cha Darajani mjini humo baada ya siku tatu za mtafaruku kutokana na kutoweka kwa Sheikh Farid.

Kutoweka kwa Sheikh Farid kulizusha ghasia kubwa mjini Zanzibar tangu Jumatano iliyopita, ambapo vijana wanaodhaniwa ni wafuasi wa kikundi cha Uamsho anachokiongoza sheikh huyo, walipambana na polisi huku askari mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) CPL Said Abdulrahman, akiuawa kwa mapanga na watu wanaodaiwa ni wafuasi wa Sheikh Farid.

Usiku wa kuamkia juzi, mtu aliyefahamika kwa jina la Salum Hasan Muhoja (30) mkazi wa Legeza Mwendo nje ya mji wa Zanzibar aliuawa kwa kupigwa risasi karibu na eneo la Amaan.

Muda mfupi baada ya kuwasili nyumbani kwake maeneo ya Mbuyuni, jana gazeti hili lilimtafuta Sheikh Farid ambaye akiwa na familia yake alieleza kuwa hakutekwa kama ilivyodaiwa, bali alichukuliwa na Jeshi la Polisi na vikosi vya usalama wakitaka kumhoji kuhusu harakati zake za kuitetea Zanzibar ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa kweli nazungumza neno kutoweka, lakini mimi sikutekwa bali nilichukuliwa na polisi. Waliniingiza katika gari na kunipeleka sehemu moja ambayo mimi nilikuwa siijui,” alisema Farid akionyesha furaha na kuongeza:

“Wakanifunga kitambaa machoni, wakanipeleka sehemu nisiyoifahamu na kuniingiza katika nyumba yenye geti nikiwa na kitambaa cheusi usoni.”

Sheikh Farid alidai kuwa mnamo saa 2:15 usiku wa kuamkia jana  alirudishwa na gari mpaka eneo walipomchukua na kushushwa kwa kusukumwa kama mzigo.

“Nilifungwa kitambaa cheusi ambacho sikufunguliwa hadi leo (juzi), walipokuja kunitupa sehemu ileile walionichukua ndipo wakanifungua,” alieleza.

Kiongozi huyo alilakiwa na viongozi wenzake wa Uamsho ambao walifika kumfariji, wakamkumbatia huku akitokwa  machozi.

Kabla ya Sheikh Farid kuonekana, viongozi wa Uamsho wakiwa na maofisa polisi walikwenda Mwangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja kuangalia kaburi, lililoonekana huko wakati hakukuwa na taarifa za kuwapo mtu aliyefariki dunia.

Naibu Amiri wa Uamsho, Azzan Khalid Hamdan alisema kuwa waliliona kaburi hilo jipya, lakini kwa vile Sheikh Farid ameonekana hakukuwa na haja tena ya kuwasiliana na Mwanasheria ili kaburi hilo lifukuliwe.

Akizungumzia hali aliyoikuta ndani ya nyumba alipokuwa ameingizwa, Sheikh Farid alisema kuwa, alifungwa kitambaa usoni na hakuweza kutembea sehemu yoyote ndani ya nyumba hiyo bali alikuwa akienda chooni na kuongeza kuwa kwa siku tatu alizokaa huko hakula chakula cha aina yoyote zaidi ya kunywa maji.

“Sikula kitu chochote kwa sababu hiyo nyumba haikaliwi na mtu lakini hata kama ningeletewa chakula nisingekula kwa vile nilikuwa siwaamini, hivyo nilipokuwa nikienda chooni kujisaidia ndiyo nilikunywa maji ya mferejini , alhamdulillah (nashukuru Mungu) amenisaidia,” aliongeza Sheikh huyo.

Alisema kuwa muda wote aliokamatwa hakuwahi kupigwa wala kudhuriwa kwa hali yoyote zaidi ya kutiwa hofu wakati akifanyiwa mahojiano.

Alieleza kuwa, kuna wakati alikuwa akihojiwa kwa hasira na ukali ili atoe maelezo yote kuhusiana na harakati zake binafsi, uhusiano wake na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad  pamoja na safari zake za kwenda Oman na kurudi.

Alisema watu waliokuwa wakimhoji walikuwa wakitofautiana kwa kuwa kila mmoja alikuwa akitumia mbinu yake huku wengine wakitumia ukali na wengine wakihoji kwa utaratibu na upole.

Alitoa wito kwa wafuasi wake kutulia na kuacha kufanya fujo, huku ombi lake kwa viongozi wa Serikali likiwa ni kutenda kwa uadilifu na kufuata kauli zao kivitendo na siyo maneno pekee.

Sheikh Farid alisema pamoja na mambo yote yaliyomtokea, kamwe hatarudi nyuma katika kuitetea Zanzibar hadi tone lake la mwisho la damu, kwani anachokifanya yeye na wenzake  kinakubalika kisheria na hakuna wa kuwazuia.

Akielekeza jinsi alivyokamatwa, alisema  awali alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mwanafunzi wake wa Madrassa ya Mahdi Mahfoudh kwamba anataka kuonana naye na kumtaka waonane katika eneo la Mbweni karibu na duka, mbele yake kukiwa na msikiti mdogo.

Alisema kuwa baada ya kupanda gari hilo, halikurudi nyuma na lilielekea njia ya Uwanja wa Ndege  na kuzunguka mzunguko wa barabara hiyo mara sita ili kumpotezea asifahamu anapopelekwa na kuanzia hapo hakuweza kujua wapi anapelekwa hadi hapo alipofika katika nyumba na kuwekwa huko kwa muda wote akiwa amefunikwa usoni.

Muda mfupi baada ya taarifa hizo kuenea kwamba Sheikh Farid ameonekana, watu mbalimbali walikuwa wakitumiana ujumbe kwa njia ya simu na facebook wakiulizia alipo ili wamwone kwa macho yao na ndipo Sheikh Farid alipotoka hapo alipoachwa na kwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa mama yake eneo la Malindi, ambapo alikutana na watu mbalimbali ambao walimshauri aende nyumbani kwake.

Muda mfupi baada ya kufika nyumbani kwake, waumini wa dini ya Kiislamu walimiminika na kukaa nje ya lango la nyumba yake wakitaka kumwona wakiwa hawaamini kama ameachiwa akiwa hai.

No comments:

Zilizosomwa zaidi