Sunday, October 21, 2012

TAMO LA SELIKARI KUHUSU VURUGU ZILIZOTOKEA HIVI KARIBUNI.

SERIKALI imepiga marufuku mihadhara ya kidini nchi nzima kwa siku 30 ikiwa ni moja ya hatua ya kukabiliana na machafuko ya kidini yanayolinyemelea taifa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alitangaza hatua hiyo ya Serikali jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Waziri Nchimbi alisisitiza  kuwa Serikali pia inafanya uchunguzi ili kubaini kama vurugu hizo zina mkono wa makundi ya nje ya nchi.
Alisema kuwa, Serikali sasa haitawabembeleza watu wanaoeneza chuki za kidini kwa sababu ni wajibu wake kulinda amani kwa wananchi wake.
Waziri huyo alieleza kusikitishwa na vurugu zilizotokea juzi Ijumaa maeneo mbalimbali jijini baada ya baadhi ya Waislamu kujiandaa  kuandamana  kwenda Ikulu kushinikiza kutolewa rumande kwa kiongozi wao, Sheikh Issa Ponda.
Waandamanaji hao pia walipinga tukio la kukojolewa kwa kitabu kitakatifu cha Kurani na mtoto lililotokea mwanzoni mwa wiki eneo la Mbagala.
“Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ametangaza juzi kusitisha mihadhara ya nje kwa siku 30. Na mimi natumia fursa hii kutangaza kusitisha mihadhara hiyo kwa nchi nzima kwa siku 30, hadi tutakapoona hali imetulia,” alisema Nchimbi.
Waziri Nchimbi alikiri pia kwamba, Serikali imekuwa ikikosea kuwakamata watu wanaofanya vurugu wakati wa maandamano na kuwaacha wanaoshawishi na kuwezesha maandamano hayo.
“Huo ndiyo uamuzi mpya wa Serikali. Anayeshawishi, anayefanikisha na anayewezesha, wote watakamatwa. Tumegundua kwamba, tulikuwa hatufuati sheria kwa kuwakamata tu wanaotenda. Ndiyo maana baada ya upelelezi tukaona kuwa wasaidizi wake (Ponda), waliwashawishi watu waandamane kwenda Ikulu ,au gerezani ili wamtoe (Ponda) rumande,” alisema Dk Nchimbi.

Katika hatua nyingine, Waziri Nchimbi alilimwagia sifa gazeti la Mwananchi kwa tahariri zake zinazohimiza kudumishwa kwa amani, hasa baada ya matukio ya uvunjifu wa amani, ikiwamo kuchomwa moto na kuibwa kwa mali za makanisa hivi karibuni.
Katika tahariri yake ya jana iliyochapishwa ukurasa wa mbele ikiwa na kichwa cha habari  ‘Chonde chonde tunaomba amani’, gazeti hili lilionya juu ya uwezekano wa kuvunjika kwa amani na likataka pande zinazohusika kujiepusha na matukio yanayoweza kulitumbukiza taifa katika machafuko.
Waziri Nchimbi alisisitiza kuwa Serikali inafuata utawala wa sheria, hivyo haitaruhusu watu kufanya maandamano kwenda popote ili kushinikiza kumtoa mahakamani mtu aliyetuhumiwa hadi mahakama itakapotoa uamuzi wake.
“Mahakama peke yake ndiyo yenye mamlaka ya kutoa hati ya mtu, hivyo kujaribu kumtoa mtu aliyefikishwa mahakamani ni kosa kisheria,” alisisitiza.
Huku akitaja mifano wa baadhi ya nchi duniani ambazo zimewahi kukumbwa na machafuko ya kidini, Dk Nchimbi alisema kuwa Serikali haitavumilia mtu au kikundi chochote kitakachoonekana kikieneza chuki za kidini.
“Staili yetu ya kucheka na wavunja amani inatuharibia. Kwetu sisi amani ni muhimu mno….Wote mnajua jinsi chokochoko za kidini zilivyoleta madhara nchini Nigeria, hakuna anayetaka kwenda tena huko, watu zaidi ya  milioni mbili waliuawa. Migogoro ya dini iliwahi kuzikumba nchi za Ulaya miaka 400 iliyopita na kusabanisha vifo vya watu milioni nne,” alisema na kuongeza:
“Huko Lebanon, Waislamu wa madhehebu ya Sunni walikuwa wakigombana na Wakristo. Hadi wanakuja kutafuta suluhisho tayari watu 250,000 walikuwa wameuawa… Hivi kweli Watanzania na sisi tutasubiri hadi watu milioni tisa wafariki, mali ziharibiwe halafu ndiyo tujadiliane?”
Dk Nchimbi amewaonya wanasiasa kutochukulia vurugu hizo kwa masilahi ya kisiasa, huku akiwataka wananchi na vyombo vya habari kutoshabikia uvunjifu wa amani.
Kuhusu vyombo vya habari vya kidini vinavyoeneza chuki alisema Serikali itaiwajibisha Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na taasisi nyingine za Serikali zinazosimamia, endapo kutakuwa na redio au televisheni na magazeti yanayoeneza maneno ya chuki za kidini.
Akizungumzia suala la kuonekana kwa kiongozi wa kundi la Uamsho la Zanzibar Sheikh Farid Hadd, Dk Nchimbi alisema kuwa baada ya kuonekana huko jeshi la polisi limemkamata na linamhoji ili kujua alikokuwa na kwa nini alipotea na kusababisha wafuasi wake wafanye vurugu iliyosababisha pia kuuawa kwa askari polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia.
Chanzo mwananchi:

No comments:

Zilizosomwa zaidi