Sunday, August 24, 2014

PINDA ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA URAIS 2015

Waziri wa Mkuu Mizengo Pinda, amevunja ukimya na kuamua kutangaza nia yake ya kutaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015.
Pinda alitangaza nia hiyo juzi usiku Ikulu ndogo ya Mwanza jijini hapa, mara baada ya kuwaalika wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) toka mikoa sita ya Kanda ya Ziwa.

Habari kutoka vyanzo vyetu vya kuaminika zilieleza kuwa Waziri mkuu aliwaalika wajumbe tisa kutoka katika wilaya zote za mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Kagera.

Pinda aliyekuwapo jijini Mwanza kwa ajili ya kuendesha harambee ya Mfuko wa Taasisi ya Benjamin Mkapa iliyofanyika jana usiku, alikutana kwa ‘mafungu’ na wajumbe zaidi ya 50 kutoka Mara, baadhi toka Mwanza, Geita na Kagera.

“Wajumbe wengine wa Shinyanga, Simiyu na wale Mwanza na Geita alikutana nao jana (juzi) jioni ili kuwashawishi wamuunge mkono  baada ya jina lake kupitishwa na NEC,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kilisema wajumbe toka wilaya hizo za Kanda ya Ziwa, walianza kuwasili Ijumaa mchana jijini Mwanza kwa lengo la kuitikia wito wa Waziri Mkuu kabla ya hawajatangaziwa nia yake.

SABABU ZA KUTANGAZA NIA
Waziri Pinda aliwaeleza wajumbe hao sababu kubwa zilizomfanya aguswe kutangaza kuwania nafasi ya Rais 2015,

ni kutokana na ushawishi mkubwa toka kwa maaskofu, masheikh, baadhi ya wabunge, watu maarufu pamoja na mke wake.
“Sikuwa na nia hiyo kwa vipindi vyote vitatu vya ubunge wangu, lakini watu hao akiwamo mke wangu, nimeshawishika kutaka nafasi hiyo,” alisema Pinda.

Alisema ameona hana sababu ya ‘kuzembea’ kutangaza nia ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu ujao.

SIFA
“Ninazo sifa za kunitosheleza kuwania nafasi hii, ikiwamo kutokuwa fisadi, pia nimekuwa ndani ya viongozi wa nchi wa awamu zote nne tangu 1974 enzi za Nyerere (Julius), Ali Hassan Mwinyi, Mkapa (Benjamin) na sasa Kikwete,” alidai.

Aidha, alisema kutokana sifa hizo hataweza kuchangishiwa pesa za kuingia madarakani kama wengine (hakuwataja), bali atawapa kiasi alichonacho ili kuwawezesha kumsaidia.

Pinda maarufu kama "mtoto wa mkulima", alidai anaamini viongozi wakuu waliopita madarakani na kuongoza nchi, wanamuunga mkono.

VIKAO VYA CHAMA
Kutokana na nafasi yake ya ujumbe wa kamati ya Maadili, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ana uhakika jina lake halitaweza kukatwa na litafikishwa katika mkutano mkuu wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama.

“Kama wajumbe wa mkutano mkuu, mjiandae ‘kunibeba’ kwani kati ya majina matano yatakayotajwa na kamati kuu, nitakuwamo na pia na kati ya matatu pia nimo…nguvu zenu ni katika mkutano mkuu.”

Ilielezwa kati ya majina matano ambayo yatapelekwa Kamati Kuu, moja ni la Pinda, mwanamke, kijana, mgombea toka Visiwani na waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa.

Hata hivyo, hofu ya Pinda ilielezwa ni baadhi ya wajumbe walioalikwa kuwa miongoni mwa wapiga debe wa baadhi ya walionyesha nia ya kugombea nafasi hiyo akiwamo Lowassa.

Aidha, habari toka ndani ya kikao hicho zilidai, wajumbe walioalikwa kuhudhuria mkutano huo waligoma kupokea mgawo wa Sh. 50,000 zilizotolewa baada ya kumalizika kwa kikao.

NAPE
Uamuzi huo wa Waziri Mkuu kutangaza nia unaenda kinyume na chama chake ambacho hivi karibuni kiliwafunga ‘midomo’ wanachama wake kutangaza nia hiyo kabla ya muda akiwamo Lowassa, Bernad Membe na Frederick Sumaye.

Juhudi za NIPASHE kumpata Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye, kuzungumzia ‘nia’ hiyo ya Pinda, zilishindikana kutokana na simu yake ya mkononi kutopatikana.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: