Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa tamko kuwa ugonjwa wa homa ya dengue umefikia hatua mbaya.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid
alisema jana kuwa kuna hali ya hatari na maambukizi ya ugonjwa huo
yanaongezeka, hivyo wananchi wanatakiwa kuwa makini.
“Kwa ufupi, mbu sasa ni hatari kuliko ilivyokuwa
awali kwa sababu hawa wanaoambukiza homa ya dengue huuma wakati wa
mchana, tofauti na wale wanaoambukiza malaria ambao huuma usiku na watu
walikwishajua kujikinga kwa chandarua au dawa,” alisema.
Waziri Rashid aliwataka wananchi kuchukua hadhari
kwa sababu ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba... “Kila mtu anatakiwa
kuchukua hatua, maji yasiruhusiwe kutuama kwa muda mrefu kwani humo
ndimo mbu huzaliana kwa wingi. Kwa mfano, maji yanayotuama kwenye kofia
za mabati, kwenye vifuu na kwenye madimbwi yanatakiwa yaondolewe ili
kuzuia mbu hao.”
Alisema ni vyema watu waende hospitali kupima
badala ya kuuchukulia kila ugonjwa kuwa ni malaria na akawataka
wasipende kutumia dawa kwa matakwa yao kabla ya kuonana na daktari.
Daktari Mtafiti katika Kliniki ya Shule ya
Kimataifa ya Tanganyika (IST), Belia Klaassen alisema tangu Januari
mwaka huu hadi jana, watu waliogundulika kuambukizwa dengue ni 203, kati
yao 110 waliugua Aprili pekee.
Alisema tatizo hilo linaongezeka kwa kuwa kuna wagonjwa 20 wapya wanaogundulika kila siku.
NIMR kufanya utafiti
Mkuu wa Kitengo cha Utafiti cha Taasisi ya Taifa
ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Julius Massaga alisema:
“Upo uwezekano wa kufanya utafiti wa tiba ya ugonjwa huo. Kwa ufupi,
huyo mbu anayesababisha homa ya dengue yupo hata hapa kwetu NIMR, kwenye
mazingira yetu.”
Dengue ilianzia IFM
Tukio la kwanza katika mfululizo kugundulika kwa
maradhi hayo lilibainika miaka mitatu iliyopita baada ya wanafunzi
kadhaa wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kufariki dunia mfululizo.
Daktari Kiongozi wa Hospitali ya Mwananyamala,
Mrisho Rupinda alisema jana kwamba wagonjwa hao walibainika mwishoni mwa
2011 na baada ya uchunguzi wa awali ilibainika kuwa idadi kubwa
waliathiriwa na dengue.
“Kwa wakati ule, wataalamu wengi walikuwa hawajajua kuwa ugonjwa
huo umeingia. Waliwapima vipimo vya kawaida na baada ya kutoona
vijidudu kama vya malaria waliwatibu kwa utaalamu wa kawaida, baada ya
vifo kadhaa ndipo ilipobainika kwamba kulikuwa na tatizo lisilokuwa la
kawaida,” alisema Dk Rupinda.
Katika hatua za awali, wataalamu walitumwa
kunyunyiza dawa kwenye eneo lote la chuo hicho na kwenye hosteli za
wanafunzi wake zilizopo Kigamboni.
Baada ya hatua hiyo, ndipo Kituo cha Utafiti wa
Magonjwa (CDC) cha Marekani kupitia kitengo chake cha uchunguzi wa
magonjwa kilipotuma wataalamu ambao kwa kushirikiana na wataalamu
wazalendo, walibaini ugonjwa huo.
Ray C apata ruhusa
Mwanamuziki Rehema Chalamila ‘Ray C’, ametoka
katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa
maradhi hayo.
Akizungumza kwa simu jana, Ray C alisema ameondoka hospitalini na yuko nyumbani baada ya kuruhusiwa na madaktari.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Sophinias
Ngonyani alisema mwanamuziki huyo aliruhusiwa baada ya kupata nafuu na
hali yake kuonekana nzuri.
Chanzo: Mwanachi
Chanzo: Mwanachi
No comments:
Post a Comment