Matokeo ya mwisho ya uchaguzi mkuu nchini Malawi yametangazwa.
Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo imemtangaza Peter Mutharika, kaka wa rais
aliyefariki dunia, Bingu wa Mutharika, wa chama cha Democratic kuwa
ndiye Rais mpya wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa matokeo hayo, Peter
Mutharika ameshinda katika uchaguzi huo kwa kujipatia asilimia 36.4 ya
kura huku Lazarus Chakwera, kiongozi wa chama cha Congress ya Malawi
akipata asilimia 27.8.
Aidha tume hiyo ya uchaguzi imemtaja Rais Joyce
Banda wa nchi hiyo kuwa, amepata asilimia 20.2 ya kura hizo. Matokeo
hayo yametolewa katika hali ambayo, mahakama kuu ya nchi hiyo imetangaza
kupinga kucheleweshwa matokeo ya uchaguzi huo wa Mei 20 mwaka huu. Hayo
yanajiri katika hali ambayo jana mamia ya watu walifanya maandamano
huko Lilongwe, mji mkuu wa nchi hiyo, wakitaka kuhesabiwa upya kura za
uchaguzi huo na kupinga matokeo hayo. Hivi karibuni Rais Joyce Banda wa
Malawi alisema kuwa, yupo tayari kuondoka madarakani iwapo mahakama kuu
ya nchi hiyo itaamua hivyo. Bado haijafahamika kama mahakama hiyo
itakubaliana na matokeo hayo ya uchaguzi, au itaamua kufuata madai ya
Bi. Banda katika kadhia hiyo.
No comments:
Post a Comment