Friday, April 11, 2014

SOKO LA MAZAO KIBAIGWA LAKABIRIWA NA UHABA WA MAZAO

20140409_080919_c051b.jpg
20140409_080925_40b11.jpg
20140409_080925_f4bc0.jpg
Soko la kimataifa la mahindi Kibaigwa katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kwa sasa ni jeupeee kutokana na kukosekana kwa mazao. Hali hii inatokana na kipindi hiki kwa cha kilimo
ambapo wananchi wengi bado 'wanatazama angani' mvua inyeshe ndipo wapate mavuno.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara waliokutwa sokoni hapo wameeleza kwamba, hali hiyo siyo ya kawaida kwa mwaka huu kwani kipindi kama hiki, licha ya wakulima wengi kusubiri mavuno shambani, mahindi huwa yanakuwepo sokoni kwa vile wapo wakulima wakubwa wanaohifadhi mahindi hata kwa misimu mitatu.
Sababu kubwa zinatajwa kwamba kuchelewa kunyesha kwa mvua na mapigano yanayoendelea kati ya wafugaji na wakulima katika maeneo ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara ambako ndiko yaliko mashamba makubwa ya mahindi, ndiko kulikowafanya hata wakulima wakubwa washindwe 'kuvunja' maghala yao kutoa mahindi ya msimu uliopita kwa kutojua hatma yao itakuwaje.
Soko hilo lililojengwa kwa gharama ya Shs. 400 milioni kuanzia mwaka 1998 linategemea sana mahindi kutoka vijiji vya Emalti, Olpopong, Laitimi, Kimana, Lembapur, Ndrigish na Mbumbuseseni ambako wakulima wamekuwa wakifukuzwa na wafugaji wa jamii ya Kimasai kwa madai kwamba wakulima hao 'wamevamia' maeneo yao ya malisho.
Hii imesababisha kuwepo kwa mapigano ya mara kwa mara licha ya wakulima ushinda kesi ya msingi waliyokuwa wameifungua tangu mwaka 2006 kupinga kuhamishwa kwa nguvu na serikali.
Tangu Januari mwaka huu, mapigano hayo yanadaiwa kusababisha mauaji ya watu zaidi ya 15 na wengine kadhaa wakiachwa na ulemavu wa maisha.
Lakini sababu nyingine inayotajwa kulifanya soko jeupe ni kutokupanda kwa bei ya mahindi, ambapo inaelezwa kwamba kwa sasa bei imeshuka tofauti na ilivyokuwa wakati wa kiangazi.
"Wakati wa kiangazi gunia moja la kilogramu 100 lilifika Shs. 60,000, lakini sasa kipindi hiki ambapo mahindi yameadimika gunia limeshuka hadi Shs. 50,000. Unadhani nani atakubali kufumua ghala lake apate hasara hasa ukizingatia wapo pia wafanyabiashara wanaonunua na kuhifadhi," amehoji Japhet Ndaiga, mfanyabiashara na mkazi wa mji huo mdogo.
Kutokuwepo kwa shughuli zozote kwenye soko hilo kumeathiri hata shughuli nyingine za uchumi kwani mji huo unategemea zaidi uhai wa soko hilo.
Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya mwaka 2012, Mji wa Kibaigwa una wakazi 24,761 ambapo kati yao wanaume ni 11,808 na wanawake ni 12,953. Idadi hii huongezeka zaidi wakati wa kiangazi ambapo wanakuwepo wafanyabiashara wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Kuwepo kwa soko hilo, ambalo ni miongoni mwa masoko machache ya kimataifa ya nafaka nchini, kumeongeza ajira kwa wananchi wengi, lakini pia kumewafanya wakulima waongeze uzalishaji kwa kupata mahindi ya chakula na ziada ndiyo hufanya biashara.

No comments: