Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wamesema kwa sasa
wanajipanga na mchezo wake ujao dhidi ya Mgambo Shooting ambapo imeahidi
kuendeleza mvua ya magoli.
Wakati Yanga ikitamba hivyo, Simba nayo imepania kuifunga Azam katika
mechi yake itakayochezwa Jumatatu. Yanga katika mchezo wake uliopita
uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam iliiadhibu timu ya Rhino
Rangers kwa magoli 3-0.
Yanga itaumana na Mgambo Shooting Oktoba 29 mchezo ambao awali
ulikuwa uchezwe kesho na ulisogezwa mbele kupisha mchezo kati ya Timu ya
Wanawake ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20 na ile ya Msumbiji
katika mchezo wao wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia
kwa Wanawake wa umri huo.
Akizungumza jana, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kiziguto alisema timu
yake iko katika hali nzuri na kama ilivyokuwa katika mchezo wao
uliopita ndio ambavyo watafanya katika mchezo ujao.
Alisema kuwa Yanga imejipanga kuhakikisha kuwa inaongoza kwa pointi katika ligi na kuongeza kuwa itahakikisha inatetea taji.
“ Kwa sasa wachezaji wapo katika hali nzuri ya kimchezo na wachezaji
wote wana nia ya kuwapa raha wapenzi wa klabu hivyo basi watu wangojee
ushindi,”alisema Kiziguto.
Kwa upande wa Simba ambao kwa sasa wana pointi 20 wakiwa sambamba na
Azam pamoja na Mbeya City wametamba kubadilisha matokeo ya sare
watakapokutana na Azam.
Simba ilitoka suluhu na Coastal Union juzi, ikiwa ni sare ya pili
mfululizo baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 na Yanga. Ofisa Habari wa
Simba, Ezekiel Kamwaga ameahidi ushindi katika mchezo huo.
Alisema kuwa wachezaji wapo katika hali nzuri ya kimchezo na kuongeza
kuwa itakuwa ni fursa yao ya kujiimarisha zaidi kileleni katika mchezo
huo.
“Ni imani yangu kuwa mchezo huo utakuwa mzuri na wapenzi wa Simba
waje wajionee namna ambavyo vijana wao wanafanya kweli na kuiongezea
pointi tatu na kuwa na pointi 23,” alisema.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment