Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe ameishutumu Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwa ni kikwazo kwake katika
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuboresha bandari ya Dar es Salaam ikiwa
nipamoja na utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).
Dk. Mwakyembe alisema watu wengi
wanaoitumia bandari ya Dar es Salaam (TPA) wanalalamikia madudu
wanayofanya TRA hasa tatizo la kufeli kwa mfumo wa mawasiliano ya
kompyuta unaotumiwa na mamlaka hiyo kutoza kodi mbalimbali.
Alitoa shutuma hizo baada ya kutakiwa
na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ajibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Watanzania
wanaofanya biashara na wale wanaoishi katika jiji la Guangzhou, jimbo la
Guangdong ambalo ni jiji kubwa la biashara lililoko kusini mwa China.
Jana usiku
(Alhamisi, Oktoba 24, 2013)Waziri Mkuu
alihitimisha ziara yake ya China kwa kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi
katika jimbo hilo maarufu kwa biashara.
Bw. Stanley Mwakipesile ambaye ni
mfanyabiashara wa Kariakoo anayefuata bidhaa zake katika jimbo la
Guangzhou, katika hoja zake alisema utoaji wa mizigo katika bandari ya
Dar es Salaam ni tatizo kubwa kutokana na mfumo wa kutoza kodi unaotumiwa na
TRA kutofanya kazi siku zingine na hivyo kusababisha mteja kutozwa fedha
nyingi.
Mfanyabiasahra huyo alisema kutokana na
kero hiyo, wafanyabiashara wengi kutoka nchi jirani wameikimbia bandari hiyo na
sasa wanatumia bandari ya Mombasa jambo ambalo alisema ni hasara kwa nchi. “Inakuwaje kila siku pale TRA system inakuwa down? Kuna urasimu mwingi tu
pale lakini cha ajabu wakati wao ndio hawafanyi kazi, lakini mteja anatozwa eti
kachelewesha kutoa mzigo,” alisema Mwakipesile.
Dk. Mwakyembe katika kujibu hoja za
mfanyabiashara huyo alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na akasema eneo
linalolalamikiwa sana ni TRA ni kuwatoza wateja tozo za ziada hata kipindi
ambacho watendaji wa mamlaka hiyo hawafanyi kazi kwa kisingizio cha mfumo
kutofanya kazi (system down).
“Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli TRA
ni tatizo, hasa hili la system down kwa kweli ni kero na linawaumiza watu
wengi wanaotumia bandari yetu. Ni lazima tukae tuone namna ya kutatua tatizo
hili,” alisema Mwakyembe.
Alisema licha ya kuwepo agizo kutoka
serikalini la kutaka TPA na TRA wafanye kazi saa 24, lakini watendaji wa
TRA wanafanya kazi kwa saa 12 tu na wanalala kwa siku 10 katika mwezi
mzima.
Alisema wakati TRA wanaenda kulala,
mteja hahudumiwi na wanapokuja kuendelea na kazi kesho yake,
wanawatoza wateja tozo ya kuchelewesha mzigo wakati makosa siyo ya
wateja bali ni ya watendaji wa mamlaka hiyo ya kukusanya kodi kwa
Tanzania.
“Sisi TPA hatulali; lakini wenzetu hawa
wanalala, inakuwaje wanaenda kulala wakati mizigo imerundikana pale bandarini?
Kwa kweli hawa watu ni lazima tushughulike nao.
“Mimi nimesaini BRN, Rais anataka kuona
mwaka 2015 shehena inaongezeka pale, na kufikia tani 18 sasa yule atakayekaa
mbele yangu kunikwamisha mie nitampitia,” alisema Dk Mwakyembe na kushangiliwa
kwa nguvu na watanzania hao.
Hata hivyo aliwatoa hofu Watanzania kwa
bandari ya Dar es Salaam inafanya kazi vizuri na kila mwaka shehena imekuwa
inaongezeka, hali inayoonyesha kuwa batu nchi nyingi ikiwemo Zimbabwe bado
zinatumia bandari hiyo.
No comments:
Post a Comment