Saturday, October 26, 2013

WADAU WAICHACHAMALIA SERIKALI KUHUSU LESENI ZA GESI

Wadau wa gesi nchini wameendelea kupinga uamuzi wa Serikali kuwaweka kando kushiriki kwenye uchimbaji wa gesi, badala yake kuwakilishwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC).
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Umoja wa Watendaji Wakuu wa Makampuni (CEOrt), Ali Mufuruki alisema hatua iliyochukuliwa na serikali itawaathiri wananchi pamoja na kampuni ya kigeni ambayo yalikuwa tayari kushirikiana na wafanyabiashara wa ndani.
“Hata wale watu wa nje ambao walikuwa wameanza kuwahusisha watu wa ndani watakuwa wameanza kujiuliza kuhusu uamuzi wao kwamba hivi tulifanya uamuzi wa busara kuwa husisha hawa, mbona viongozi wao wanasema hawafai? Hii si sawa,” alisema Mafuruki na kuongeza:
“Hakuna nchi duniani ambayo imesimama na kusema kuwa watu wa ndani wasihusike kwasababu hawana uwezo, pesa na ni mafisadi.”
Kauli ya watendaji hao inakuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi (TPSF), Dk Reginald Mengi kupinga msimamo wa serikali kuwa wafanyabiashara wa ndani hawana uwezo wa kuchimba gesi kutokana na kuwa na mitaji midogo.
Pia Mafuruki alipinga ufafanuzi uliotolewa juzi na Rais Jakaya Kikwete kuwa sekta binafsi itafuata masharti sawa na wawekezaji wa nje na kusema kuwa hatua hiyo inalenga kuwakandamiza wazawa.
“Haiwezekani sera ambayo inasimamia uendelezwaji wa hii sekta ikawa inasema kwamba wawekezaji wa nje na ndani wawe sawa, hakuna kitu kama hicho,” alisema.
Alisema utafiti unaonyesha kuwa nchi za Saudi Arabia, Marekani, China, Nigeria, Malaysia na Norway zinatoa kipaumbele na ulinzi kwa wawekezaji wa ndani katika sekta ya madini na nishati kutokana na umuhimu wake katika kukuza uchumi wa nchi.
Mwenyekiti huyo alisema TPDC haina uwezo wa kushiriki uchimbaji wa gesi, ila imepewa nafasi hiyo kwa kuwa ni shirika la umma na kwamba sheria inataka iwe hivyo.
“Kwa nini Serikali ibague, au kwasababu TPDC ni shirika la umma? Sawa wao washiriki lakini na sekta binafsi waruhusiwe… kutumia kampuni moja ni kujiweka kwenye hatari, kwa sababu linaweza kufa na hakuna ambaye anaweza kuniambia haiwezi kufa,” aliongeza.
Alipendekeza kuwepo kwa sheria za upendeleo kwa wazawa katika sekta mbalimbali ili kuwanufaisha wadau wengi zaidi.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Santina Benson alisema lazima serikali ijifunze kutokana na makosa kwa kuangalia sera ya madini ambayo imeshindwa kuwanufaisha Watanzania wote.
“Hatuwezi kuiacha historia ijirudie yenyewe. Tunahitaji kuangalia nyuma miaka 20 iliyopita wakati sera ya madini ilipokuwa inatungwa.
Watanzania hawajanufaika nayo huku wengi wakiwa bado wanaishi chini ya mstari wa umaskini,” alisema na kuongeza kuwa:
“Ni ukweli uliowazi kwamba sera ya madini ilishindwa kulinda rasilimali za Watanzania kwa hiyo safari hii lazima tuhakikishe tunafanya vizuri.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Zilizosomwa zaidi