Saturday, October 12, 2013

TANZANIA DAIMA: ZITTO AFICHUA MBINU CHAFU

Zitto kabwe
 
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe amesema kuna njama inayofanywa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutaka mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya usiishe ili wajiongezee muda hadi mwaka 2017.

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema kuwa lengo la wabunge hao ni kutaka muda wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 usogezwe mbele hadi 2017 ili waendelee kukaa madarakani.

Alisema kuwa CHADEMA haitakubali uvunjwaji wa aina yoyote wa katiba, na hivyo kumtahadharisha Rais Jakaya Kikwete kutothubutu kukubaliana na fitna hizo.

Madai ya Zitto yaliwahi pia kutolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alisema kuwa CCM wanataka kukwamisha mchakato wa katiba makusudi ili kutengeneza sababu ya kuongeza muda wa Rais Kikwete kubaki madarakani kwa miaka miwili zaidi.

Prof. Lipumba alisema kuwa hoja ambayo CCM wanataka kuitumia kukwamisha mchakato huo, ni muundo wa serikali ambapo dakika za mwisho wanataka kukubali serikali tatu kisha watumie kisingizio cha uundwaji wa taifa la Tanganyika kuchelewesha katiba mpya.

Akihutubia mikutano mbalimbali ya hadhara katika Jimbo la Bukene mkoani hapa, ukiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya ujenzi wa chama katika Kanda ya Magharibi jana, Zitto alisema hata vurugu zilizotokea bungeni hivi karibuni na Naibu Spika Job Ndugai, kuruhusu askari waingie ndani ya Bunge kuwakamata na kuwapiga wabunge wa upinzani, ilikuwa ni sehemu ya mpango huo wa kutaka kusogezwa mbele kwa muda wa wabunge kutoka madarakani.

Zitto alifafanua kuwa hoja inayojengwa na wabunge hao ambao wameshaanza kuipenyeza kwa ajili ya kumfikia Rais Kikwete, ni kwamba kama katiba mpya itapatikana kwa wakati huu, muda wa kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2015 utakuwa hautoshi.

“Hawa ni wabunge waroho wa madaraka, hawajafanya jambo lolote jema katika majimbo yao, na sasa wanajua hawawezi kurudi ndiyo maana wanataka muda usogezwe na wao waendelee kulipwa mshahara na posho.

“Sisi CHADEMA tunasema hilo hapana, hatuwezi kukubali uchaguzi usogezwe kwa miaka miwili, na namuonya Rais Kikwete asithubutu kuingia katika mkenge huo unaowahusisha baadhi ya mawaziri,” alisema.

Aliongeza kuwa wananchi waliwachagua wabunge wao kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitano, na kwamba kuwe na katiba mpya au isiwepo ni muhimu uchaguzi kufanyika ili wale walioshindwa kuwajibika wakae pembeni.

Zitto alisema CHADEMA inatoa kauli hiyo ili wananchi wajue mkakati huo, na washiriki kuupigia kelele, kwa kile alichoeleza kuwa mipango hiyo imeshaanza jijini Dar es Salaam na Dodoma.

Kwa mujibu wa Zitto, baadhi ya mawaziri wanataka kutumia nafasi ya kuwa karibu na rais ili kumshawishi akubali mkakati huo, kwa kumueleza kuwa hali hiyo itamjengea heshima na kumbukumbu ya kuiachia nchi katiba iliyo bora.

Avunja ngome ya CCM
Katika hatua nyingine, Zitto ameitikisa ngome ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi.

Dalili ya ngome hiyo kutikiswa ilianza kuonekana mapema wiki hii wakati viongozi wa CHADEMA Wilaya ya Uyui walipokuwa wakifanya maandalizi ya mkutano katika Kata ya Mabama, ambako ni nyumbani kwa kigogo huyo.

Baada ya kutangazwa kuwapo kwa mkutano wa CHADEMA katika kata hiyo, gazeti hili lilishuhudia jitihada mbalimbali za viongozi wa CCM zikifanyika, ikiwemo kuweka bendera mpya kila baada ya nyumba mbili, huku zile nyumba za wakazi wasiokuwa wafuasi wa chama hicho, zikiwekwa barabarani.

Baadhi ya wakazi wa kata hiyo na maeneo mengine ya jirani ambao walijitokeza kumsikiliza Zitto, walieleza kuwa baadhi ya nyumba zilizowekwa bendera wakazi wake walitishiwa kufanyiwa hujuma kupitia ofisi ya mtendaji wa kata hiyo endapo wangekataa.

“Unaona bendera zote ni mpya, hapa tumewachoka, na sasa wanatumia vitisho kutaka kuweka bendera zao kwenye nyumba zetu,” alisema mmoja wa wakazi hao ambaye hakutaka kutajwa jina.

Hata hivyo, mkutano wa Zitto nusura uingie dosari baada ya msafara wake kuchelewa kufika katika Kata ya Mabama, kisha mtu aliyejitambulisha kama ofisa mtendaji wa kata hiyo, kuwataka wananchi watawanyike kutoka katika uwanja wa mkutano.

Lakini wananchi hao hawakukubaliana na agizo hilo na kuahidi kumsubiri Zitto ambaye aliwasili katika eneo la mkutano saa 12:47 jioni na kuwahutubia hadi saa moja na robo usiku.

Kabla ya kuhutubia mkutano huo, Zitto aligawa kadi kwa wanachama wapya waliotoka CCM na kuwataka wasiogope vitisho vyovyote vinavyofanywa na viongozi wa chama hicho.

Alisema CCM imeua njia ya reli iliyokuwa ikiwasaidia wakazi wa Mabama kufanya shughuli za kila siku za kujipatia kipato.

Hata hivyo, Wakasuvi alikanusha chama chake kujihusisha na vitendo vya kuwatisha wananchi, akisema kuwa wao wanatumia nguvu ya hoja.

No comments:

Zilizosomwa zaidi