Wednesday, October 9, 2013

NUKUU ZA WANASHERIA WANAOMPINGA TUNDU ANTIPAS LISSU KUHUSU KUTIA SAINI MUSWADA WA KATIBA MPYA

Baadhi ya wanasheria wameunga mkono utaratibu wa  Rais kutia saini Muswada wa  Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, uliopitishwa hivi karibuni na Bunge kwa hoja kwamba umepitia   mchakato sahihi na halali wa Kikatiba.

Wanasheria hao wakaeleza kumshangaa mwanasheria mwenzao na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), kwa ushauri wake alioutangaza kwa umma, kumtaka Rais asisaini muswada huo, kwamba ushauri huo ni wa 
kisiasa zaidi, usio na tija kwa uongozi wala unaofuata utaratibu na sheria.

Wamenukuliwa wakizungumza na mwandishi kwa nyakati tofauti jana, wakisema kuwa muswada huo kama ilivyo miswada mingine ya sheria, una nafasi ya kusainiwa na yakiwepo marekebisho, unarudishwa bungeni kujadiliwa na kurekebishwa.

Wakili wa kujitegemea, John Mapinduzi alisema: "Lazima muswada huo usainiwe ndipo urudishwe bungeni kwa marekebisho, Lissu ni mwanasiasa tu anapotosha umma… sasa utarudishwaje bungeni wakati ulishapita?" Alihoji Mapinduzi.

Mwanasheria mwingine wa kujitegemea, Jerome Msemwa alisema kusainiwa muswada huo ni njia sahihi na inafanyika mara nyingi (??) na kama kuna marekebisho, yanafanyika baadaye: "Wabunge kama Lissu waliamua kutoka wenyewe bungeni wakati muswada unajadiliwa… hakuna aliyewafukuza, sasa iweje leo watake usisainiwe? Haina maana leo hii kumshauri Rais kutosaini. Ushauri wa Lissu, kisheria hauna maana yoyote, hawezi kumshauri Rais leo asisaini wakati anafahamu kuwa hata baada ya kusainiwa, kuna nafasi ya kurudishwa bungeni na kujadiliwa kwa marekebisho yoyote," alisema Msemwa.

Msemwa alisema Rais asiposaini muswada huo na kuurudisha bungeni, maana yake vikao vya wabunge vilivyokaa Dodoma  kujadili muswada huo, vilipoteza muda na fedha za wananchi bure.  
Chanzo: Habari Leo

No comments:

Zilizosomwa zaidi