Gari likiwa limepinduka bondeni. |
Mwimbaji anayetamba na wimbo wa "Zawadi gani nitamtolea BWANA" ambaye
pia ni mtume akichunga kanisa jijini Dar es Salaam John Komanya amepata
ajali mbaya juzi mchana maeneo karibu na daraja la Mto Wami akiwa njiani
kuelekea mkoani Arusha kukutana na viongozi wanaohudumu na mwalimu
Christopher Mwakasege, kwa ajili ya mkutano wa injili ambao utakuwa na
lengo la kuombea taifa kwa siku nne mwezi Disemba.
Akizungumza na GK mtume Komanya amesema lengo lilikuwa ni kupeleka barua
kwa viongozi hao ili wamfikishie mwalimu Mwakasege kwaajili ya mkutano
huo. Amesema akiwa njiani katikati ya Msata na Wami na wakati huo hakuwa
amefunga mkanda wa gari, ndipo akasikia sauti ya Roho Mtakatifu
ikimwambia kwa upole afunge mkanda lakini akawa anapuuzia na kuanza
kujiuliza kwanini, sauti ikarudia tena kwa upole ikimwambia afunge
mkanda akiwa bado anajiuliza ndipo anasema akasikia sauti ya Mungu
ikizungumza kwa haraka na ukali "John funga mkanda" ndipo akafunga
mkanda.
Mtume Komanya amesema akiwa anateremka kuelekea wami akiwa katika mwendo
wa 180 wakati akipita katika kona kulikuwa na malori matatu mbele yake
kukawa na lori lingine likifuatiwa na mabasi matatu yakipandisha kutoka
Arusha kuja Dar, kwa wakati huo aliona malaika saba ambapo walishuka
mithili ya makomandoo washukavyo kutoka kwenye kamba ya helikopta, mmoja
akiwa amekaa kwenye boneti mbele, mwingine kulia, kushoto na mwingine
nyuma yake ambaye alimwambia Komanya afuate maelekezo yake, anasema
akiwa anamwangalia malaika aliyekaa karibu naye katika kiti cha dereva
aliambiwa afuate maelekezo anayopewa na malaika wa nyuma yake.
Alipokuwa akiangalia mbele akaona gari linayapita mengine kwa spidi hali
iliyomfanya Komanya kutaka kuingia katikati ya magari mengine lakini
malaika akamwambia afuate maelekezo yake na kuambiwa aachie uskani jambo
ambalo alilipinga kwakuwa aliona kifo mbele yake na kutaka kuingia
katikati ili kukwepa, lakini malaika akamwambia ukiingia katikati
utakufa, wewe achia usukani kama ninavyokwambia kwakuwa wametumwa
kumlinda, akawa bado anatafakari kutokana na kuliona korongo kubwa
upande wake huku malaika wakimwambia asiguse kitu chochote ikiwemo
kutokanyaga breki lakini bila kusikia akakanyaga na kusababisha gari
kuyumba sana, malaika akamwambia tena aachie breki na kuweka mikono yake
kifuani. Anasema alipoweka mikono kifuani aliona wakiligonga lori huku
malaika akiwa ameshika usukani na kuonyonga sana huku yeye akisema
alijikuta akiwekwa kwenye kitu kama chupa ya maji, na yeye kwa wakati
huo kuona kama vile yupo ndani ya glasi ya maji, ila anaona
kinachoendelea.
Kisha baada ya hapo, upande wake wa usukani ndio uliogongwa, mara baada
ya malaika kuchezesha usukani kidogo ili kuepusha madhara zaidi, na
kisha ile semi-trailler ikamtupia kwenye korongo na kubinuka mara tatu
hewani kabla ya kutua chini kwa mara ya nne, ambapo gari ilikuwa juu
chini, yaani matairi yakiwa yanatazama juu.
Baada ya hapo kilichofuata ni kuendelea kusikiliza malaika wasemacho,
ambapo hapo alisikia sauti ikisema fungua mkanada utoke, na kwa wakati
huo kulikuwa na moshi ullioanza kutoka kwenye gari - na hapo akapewa
dakika 12 kuchukua baadhi ya vitu alivyokuwa navyo kwenye gari. Maajabu
ya Mungu, hakuna kitu chochote kilichogusa mwili wake, na wala hakuna
damu iliyovuja kutokana na gari hilo kupindukia kwenye korongo.
Hakika utukufu ulimrudia Mungu kwa wakati huo kwani baadhi ya mashuhuda
walikiri hapohapo ya kwamba hakuna mtu anayeweza kusalimika kwenye ajali
hiyo, bali ni lazima tu mkono wa Mungu umehusika hapo kuokoa.
Baadhi ya mashuhuda ambao walikuwapo kwenye mabasi ya mkoa (hadi mkoa)
walimtambua mtumishi wa Mungu ya kwamba ni John Komanya na hatumaye
kumshukuru Mungu hapohapo, ambapo baadae Polisi walifika kwa ajili ya
kazi yao - lakini hilo halikumzuia Mchungaji Komanya kupiga magoti na
kumshukuru Mungu licha ya umati wa watu - na tukio hilo liliambatana na
yeye kuisikia sauti ya Mungu ikimwambia "Nimekupa kazi ya kutengeneza kanisa langu,... usiogope nitakulinda, ila kuwa mwaminifu na nitakuweka kwenye uaminifu"
Sauti hiyo ilitoka kwa kiumbe ambacho kilikuwa na muonekano wa malaika,
Pastor Komanya anaieleza GK na kusema kuwa sauti yake ilikuwa ya
tofauti, na mavazi yake yalikuwa ni meupe na kwamba alielezwa dhahiri
kuwa hiyo semi trailer ilikuwa imetumwa kummaliza, lakini ndio maana
malaika walitumwa kumlinda.
"Zawadi Gani" kama ambavyo alikuwa akiitwa akiwa hospitali ya Muhimbili,
alifanyiwa vipimo na kuonekana ya kwamba hana shida yoyote. Na hili
linadhihirika hata pale alipotoka kwenye gari lililopiinduka, kwa kuwa
alitoa vifaa vyake na kuanza pia kupiga picha, picha ambazo kama mtu
akiziona zote, hakika hawezi kuamini kama kuna kusalimika hapo.
Mwisho wa yote Mchungaji Komanya anakiri kuwa amepona kwa rehema ya
Mungu, na baada ya hapo amemuahidi kumtumikia kwa kazi aliyompa licha ya
kwamba ni ngumu na ina vikwazo vingi. Jumapili hii, Mchungaji Komanya
ataimba wimbo mpya kumshukuru Mungu kutokana na kumuepusha na kifo. Kwa
wasafiri wote, hapa kuna funzo la kujikabidhi mikononi mwa BWANA kila
mara safari inapotokea, katu tusienende kwa mazoea.
No comments:
Post a Comment