Saturday, October 12, 2013

DADA WA NYUMBANI AMUUA MTOTO WA BOSI WAKE NA KUMTUMBUKIZA KWENYE DIMBWI LA MAJI MACHAFU


Hausigeli aliyejulikana kwa jina moja la Ester (14) yupo matatani kwa madai ya kumuua mtoto Arafat Allan (3) kwa kumnyonga shingo na kumpiga na kitu kizito kichwani kisha kuutumbukiza mwili wake kwenye dimbwi la maji machafu.

Tukio hilo lilijiri Jumapili iliyopita Mailimoja, Kibaha mkoani Pwani ambako marehemu alikuwa akiishi na wazazi wake.

Akizungumza kwa uchungu, mama mzazi wa mtoto huyo, Zakia Peter ambaye amelazwa katika Zahanati ya Kellen kutokana na mshtuko wa kifo cha mwanaye, alisema siku ya tukio, hausigeli huyo aliyekuwa na siku mbili tangu aanze kazi aling’ang’ania kutumwa sokoni saa mbili asubuhi ambapo alimkubalia na kumuagiza mboga.

Bila mwanamke huyo kujua, msichana huyo alimpitia Arafat kwa jirani alikokuwa akicheza na wenzake na kuondoka naye kwa madai anamsindikiza.
 
“Nilipoona muda unasonga mbele bila hausigeli kurudi na mtoto nilianza kuwatafuta,” alisema mama wa marehemu.
Akasema aliwatafuta kwa muda mrefu bila mafanikio mwishowe yeye na majirani zake wakaenda kutoa taarifa polisi na kufunguliwa jalada la kesi KB/RB/1154/2013 TAARIFA.

Mama wa marehemu aliendelea kusema kuwa zoezi la kumsaka msichana huyo na mtoto wake liliendelea mpaka Jumanne iliyopita ambapo habari zilisambaa kwamba kuna maiti ya mtoto wa kiume  imekutwa ikielea kwenye dimbwi la maji machafu linalotumika kumwagilia bustani za mboga maeneo hayo.
 
 Mama  mzazi  akiwa  hospitalini baada  ya kuzimia


“Niliondoka na ndugu wengine hadi kwenye dimbwi hilo! Nilipata mshtuko mkubwa kukuta maiti ya mtoto anayeelea ni ya mwanangu Arafat,” alisema huku machozi yakimtoka.
Baada ya hapo, mwili huo ulipelekwa katika Hospitali Teule ya Tumbi, Kibaha ambapo madaktari waliufanyia uchunguzi na kubaini kuwa marehemu alinyongwa shingo na kupigwa na kitu kizito kichwani hali iliyomsababishia mauti.

Baadhi ya watu waliozungumza nasi   akiwemo mama wa marehemu, walisema kwa siku mbili hizo alizofanya kazi hausigeli huyo alionekana kuwa na mambo ya kishirikina kwani asubuhi ya siku ya tukio aliamka akiwa amenyolewa nywele upande mmoja.
 
“Siku hiyo ya Jumapili huyo mdada wa kazi aliamka akiwa amenyolewa nywele upande mmoja, alipoambiwa amalizie zote alikataa akisema atanyoa baada ya kutoka sokoni ambapo hakurudi tena,” alisema mama wa marehemu.
Jumatatu iliyopita, siku moja baada ya tukio, hausigeli huyo alikutwa akirandaranda stendi akiomba fedha za nauli ili arudi kwao Mbeya lakini alikamatwa na kufikishwa kwenye kituo kidogo cha polisi.

Habari zinasema hali kwenye kituo hicho ilikuwa mbaya kufuatia baadhi ya wakazi wa eneo hilo kujaribu kukivamia ili wamuue mtuhumiwa huyo. Ilibidi mtuhumiwa ahamishiwe Kituo cha Polisi cha Tumbi, Kibaha.
Kwa mujibu wa watu wa karibu wa familia hiyo, msichana huyo aliokotwa na ndugu wa baba wa marehemu baada ya kumkuta barabarani akiomba msaada akidai anateswa na ndugu zake, wakampeleka kwa baba wa marehemu ili wamsaidie ambapo walimpa shughuli ya kazi za ndani.

Baba wa marehemu, Allan hakuweza kuzungumza kutokana na kuwa kwenye hali mbaya katika Zahanati ya Kellen alikolazwa baada ya mwanaye kuzikwa katika Makaburi ya Mailimoja, Jumatano iliyopita.

No comments:

Zilizosomwa zaidi