Wanamgambo waliokuwa wamevaa nguo za kijeshi,
wamewaua watu 19 katika kuzuizi cha barabarani walichokuwa wameweka
kukagua magari katika jimbo la Borno.
Wanaume hao waliokuwa wamejihami,
waliwasimamisha madereva na kuwaamrisha kuondoka kutoka katika magari
yao kabla ya kuwapiga risasi na kuwaua.
Walioshuhudia tukio hilo waliambia
BBC kuwa wanaume hao walikuwa wanachama wa Boko Haram, ingawa kundi hilo
bado halijatamka chochote kuhusu mauaji hayo.
Jimbo hilo la Kaskazini mwa Nigeria liko chini
ya sharia ya hali ya hatari, huku Boko Haram wakiwa vitani na serikali
kutaka utawala wa kiisilamu.
Kundi hilo huwalenga raia na wanajeshi kwa mashambulizi ikiwemo shule na makabiliano ya mara kwa mara na jeshi la taifa.
Shambulizi la hivi karibuni, lilifanyika
jana Jumapili asubuhi karibu na mji wa Logumani, ambao hauko mbali sana na
mpaka na Cameroon.
Walionusurika shambulizi hilo walisema kuwa
washambuliaji walivaa nguo za jeshi na walikuwa wanaendesha pikipiki
kabla ya kuwashambulia waathiriwa.
"Takriban wanaume 9 walituamuru kuondoka kwenye magari yeu na kulala chini,’’ alisema mwanamume.
"Waliwaua watu 5 kwa kuwapiga risasi na kisha
kuwanyonga wengine 14 kabla ya mtu mmoja kuwapigia simu na kuwambia kuwa
wanajeshi wanakuja.’’
Alisema washambuliaji baadaye walitoroka na kujificha msituni kwa pikipiki zao.
Manusura mwingine alisema kuwa alisikia mtu
aliyekuwa karibu naye akiuawa kwa kisu. Alisema ana uhakika kuwa
washambuliaji walikuwa Boko Haram kwa sababu ya kuwa na ndevu.
Mwandishi wa BBC Tomi Oladipo alisema kuwa ni
jambo la kawaida kwa polisi kuweka vizuizi barabarani hasa katika maeneo
yenye misukosuko na huenda washambuliaji waliiga mbinu hioyo ya jeshi
ili kuwanasa waathiriwa.
Boko Haram limezua mgogoro mkubwa wa kisiasa
Nigeria tangu mwaka 2009 ambapo nia yao kuu imekuwa kuunda utawala wa kiisilamu,
hasa katika maeneo ya kaskazini mwa nchi.
Kundi hilo limelaumiwa kwa mashambulizi kadhaa ambao yamesababisha takribana vifo 2,000 tangu mwaka 2011.
BBC Swahili
No comments:
Post a Comment