Katazo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na Meja Erick Komba
wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya mgogoro
huo.
Alisema hali hiyo inatokana na jeshi hilo kubaini kuwa baadhi ya
vyombo vya habari nchini vinaandika habari za uchochezi zinazotaka
kuziingiza vitani nchi ya Tanzania na Rwanda.
Meja Komba alisema hategemei kama kutakuwa na chombo chochote cha
habari kitakachotoa habari kuhusu maendeleo ya mgogoro huo bila kupata
taarifa rasmi kutoka jeshi hilo.
Alionya kuwa chombo chochote kitakachokwenda kinyume kitakuwa kina tatizo.
Meja Komba alisema wananchi wanapaswa kuelezwa kuwa kikosi cha
Tanzania kilichoko DRC ni sehemu ya Brigedia ya SADC, iliyotoa mchango
wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa (Monusco).
Alitaja majukumu ya kikosi hicho kuwa ni kuzuia waasi wa M23 na
wengine kujitanua, kuvunja nguvu zao na kuyapokonya silaha makundi yote
ya waasi.
“Kwa kuzingatia kuwa kikosi chetu kiko chini ya majeshi ya Monusco,
inamaanisha kuwa operesheni hiyo ni ya Umoja wa Mataifa,” alisema.
Aliongeza kuwa Tanzania haikupeleka kikosi chake DRC kwa ajili ya
kupigana na M23, pia ieleweke kuwa haina tatizo na Rwanda kuhusiana na
operesheni hiyo ambapo Rwanda ilitoa ridhaa kikosi cha Tanzania kwenda
DRC.
Meja Komba alisema Rwanda ni miongoni mwa wanachama wa nchi za Maziwa
Makuu, ambayo imesaidia kwa kuruhusu kikosi cha Tanzania kupitisha vifaa
na zana katika nchi yake kupeleka DRC.
“Tanzania inashiriki katika operesheni hiyo ya ulinzi wa amani nchini
DRC kutokana na mgogoro kati ya serikali na waasi hususan kikundi cha
M23,” alisema.
Mgogoro huo ulianza Aprili mwaka jana, ambapo kikundi cha M23
kilijitoa katika jeshi la serikali na kuanzisha mapigano yaliyosababisha
hali ya usalama nchini DRC kuwa mbaya.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe Benard, amesema kuwa marais Jakaya Kikwete na
Paul Kagame wa Rwanda wamemaliza tofauti zilizokuwa zimejitokeza kati
yao hivi karibuni.
Marais hao walikutana na kufanya kikao cha faragha jijini Kampala
nchini Uganda juzi baada ya mkutano wa viongozi wa nchi za Maziwa Makuu
na baadaye kutoa taarifa kwa waandishi wa habari.
Kuzorota kwa mahusiano kati ya viongozi hao kulikuja kufuatia kauli ya
Rais Kikwete ya kumtaka Rais Kagame kukaa meza moja na vikundi vya
waasi wa nchi yake vilivyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,
ushauri ulioonekana kumkera Rais Kagame.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Membe
alisema marais hao walitumia mazungumzo yao yaliyochukua muda wa saa
moja kujadiliana na kueleweshana mambo mbalimbali yaliyosababisha
kutoelewana.
“Baada ya mkutano huo ambao uliwapa fursa za kuchambua, kujadili na
kurejesha mahusiano ya kihistoria kati ya nchi hizi mbili, marais wetu
walitoka na nyuso za furaha,” alisema.
Moja ya maazimio ya kikao chao ni kuwa na vikao vingine kati ya Rwanda na Tanzania katika siku zijazo.
“Kwa kweli kikao kati ya Rais Kikwete na Rais Kagame kimeondoa majungu
yote, kimekata fitina, uongo na maneno ya kuchombeza yaliyokuwa
yakitawanywa na watu mbalimbali hapa nchini na hata kule Kigali,”
alisema.
Mbali ya kikao hicho pia Rais Kikwete alifanya kikao kingine cha
faragha na Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambapo walipata muda wa
kujadiliana kwa kina kuhusu mambo mbalimbali kuhusu nchi zao na mambo ya
migogoro katika nchi za Maziwa Makuu.
Akizungumzia yale yaliyokubaliwa katika mkutano wa viongozi wa nchi za
Maziwa Makuu, Membe alisema kuwa mkutano huo kwanza ulimruhusu Rais
Museveni aendelee kusuluhisha vita ya serikali ya DRC na waasi.
Alisema kuwa viongozi hao walilaani mashambulizi ya M23 yaliyojeruhi
na kumuua Meja Mshindo wa Tanzania aliyekuwa miongoni mwa askari walioko
nchini Congo katika kusimamia amani chini ya Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment