Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limetibitisha kuwa kiongozi
wao Ahmed Abdi Godane aliuawa siku ya Jumatatu katika shambulizi la anga
lililotekelezwa na jeshi la Marekani.
Msemaji wa kundi hilo amesema kuwa wanachama wengine wawili wa kundi
hilo pia waliuawa katika shambulizo hilo lililotekelezwa kilomita 170
kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu.
Kwa mujibu wa BBC, kundi la Alshabaab limemchagua kiongozi mpya,
Ahmad Omar katika mkutano uliofanyika katika eneo lisilojulikana.
Hata hivyo, ripoti zisema kuwa kiongozi huyo mpya hajulikani vyema.
Kufuatia kuuawa kwa kiongozi huyo, hofu imetanda nchini humo hususani
kwa raia wanaoamini kundi hilo linapanga njama ya kulipiza kisasi.
Bado haifahamiki kama Ahmad Omar ataendeleza sera za Godane za
kuwalenga viongozi wa serikali ya Somalia na kufanya mashambulizi ya
kushitukiza katika maeneo mbalimbali nchini Kenya au atakuwa na mbinu
mpya.
Bado Alshabaab inashikilia eneo kubwa kusini mwa nchini hiyo.
Serikali ya Somalia imeeleza kuwa imejidhatiti kujilinda na jaribio lolote la Alshabaab.
No comments:
Post a Comment