Tuesday, September 24, 2013

TAARIFA KUTOKA IKULU YA NCHI DSM KWENDA KWA WATANZANIA WOTE

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425



PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Hakuna uporaji wa ardhi ya wakulima wadogo unaofanywa na Serikali – JK

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hakuna uporaji wowote wa ardhi unaofanywa na Serikali yake dhidi ya ardhi ya wananchi na hasa wakulima wadogo.

Aidha, Rais Kikwete amesema Serikali ya Tanzania haiwezi kupora ardhi ya wananchi na hasa wakulima wadogo kwa sababu sera za kilimo za Serikali zinalenga kumlinda mkulima mdogo na kumwezesha kujikomboa kutoka kwenye umasikini.

Rais Kikwete alitoa msimamo huo, kwa mara nyingine tena, mwishoni mwa wiki wakati alipozungumza na wana-jumuia ya Chuo Kikuu cha Guelph cha Toronto, baada ya kuwa ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima ya Sheria na Chuo hicho maarufu cha Canada.

Katika hotuba yake ya kupokea na kukubali shahada hiyo, Rais Kikwete ambaye alizungumzia maendeleo na changamoto za kilimo katika Afrika alisema kuwa kamwe Serikali ya Tanzania haiwezi kupora ardhi ya wakulima wadogo wadogo kwa sababu sera ya Serikali katika mipango yote mikubwa ya kilimo ni kumlinda na kumtetea mkulima mdogo.
           
“Hakuna uporaji wa ardhi unaofanywa na Serikali katika Tanzania kama inavyodaiwa na baadhi ya watu. Uporaji wa ardhi ya mkulima mdogo hauwezi kutokea katika Tanzania kwa sababu sera za Serikali ni kuhakikisha kuwa mkulima mdogo anakuwa mtu wa kwanza kunufaika na kufaidika na sera za kilimo za Serikali,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Mkulima mdogo yuko katikati ya mipango na sera za Serikali, na kwa kweli ndiye mtu muhimu zaidi katika mipango ya kilimo ya Serikali.  Kazi ya wakulima wakubwa ambao tunawakaribisha kuwekeza katika Tanzania ni kuunga mkono shughuli za kilimo za wakulima wadogo kwa maana kweli kweli ya uwezeshaji.”

Rais Kikwete amesema kuwa kwa kadri Serikali inavyokaribisha wakulima wakubwa kuwekeza katika kilimo na uchumi wa Tanzania, ni dhahiri kuwa Serikali itaendelea kuwalinda na kuwatetea wakulima wadogo ambao watashirikiana na wakulima wakubwa katika kuboresha kilimo cha Tanzania.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

23 Septemba, 2013

No comments:

Zilizosomwa zaidi