Tuesday, September 24, 2013

NCHIMBI AWATAKA WANANCHI KUCHUKUA HADHARI DHIDI YA WAGENI

Waziri Emmanuel Nchimbi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi amewataka Watanzania kuchukua hadhari dhidi ya raia wa kigeni wakati huu ambao amani ya dunia ipo shakani.
 
Tamko hilo limekuja wakati kundi la kigaidi la Al-Shabaab limevamia jengo kubwa la biashara la Westgate huko Nairobi, Kenya na kuua zaidi ya watu 60 huku mamia wakijeruhiwa na wengine kadhaa kuendelea kushikiliwa mateka tangu Jumamosi iliyopita.
Hata hivyo, Dk Nchimbi hakugusia tukio hilo kwenye maelezo yake lakini aliwataka Watanzania waache tabia ya kuwapa hifadhi raia wa kigeni akisema ni hatari kwa usalama wa taifa... “Watanzania lazima tuwe makini hasa nyakati hizi ambazo usalama wa dunia upo shakani.”
Alisema Serikali kwa upande wake, imekuwa ikijitahidi kuweka nchi katika hali ya usalama ikiwa ni pamoja na kuendesha operesheni za kuwasaka wahamiaji haramu.
“Hakuna uhalali wa mtu kukaa katika nchi nyingine bila kufuata taratibu za sheria,” alisema na kuongeza: “Ni lazima vyombo vya usalama kujua nani kaingia na nani anaondoka.”
Alisema operesheni inayoendelea ya kuwabaini na kuwachukulia hatua wahamiaji haramu inayojulikana kwa jina la Kimbunga, waziri huyo alisema imebainika kuwa baadhi ya Watanzania wanawahifadhi raia wanaoishi nchini kinyume cha sheria.
Alitoa mfano wa raia wa Uingereza ambaye alikuwa akitafutwa na nchi yake kutokana na vitendo vya kigaidi lakini akakamatwa akiwa amehifadhiwa na Mtanzania ambaye alikwishamfanyia mipango ya kupata vitambulisho kama kile cha mpiga kura.
Alisema mkakati wa kuwaondoa raia wa kigeni ulianza Julai 26, mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alipotoa kipindi cha wiki mbili watu wanaoishi nchini kinyume cha taratibu kuondoka kwa hiari yao.
“Katika agizo hilo la Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, raia wa kigeni 21,758 waliondoka na kurejea makwao kwa hiari,” alisema.
Dk Nchimbi alisema operesheni ya kuwaondoa wale ambao hawakutii amri ya Rais Kikwete ilianza Septemba 6, mwaka huu na hadi ilipomalizika wiki hii, watu 12,604 walikuwa wametiwa mbaroni.
“Kati ya hao Wanyarwanda ni 3,448, Warundi 6,125, Waganda 2,496, Wakongo 589, Wasomali 44, Myemeni mmoja na Mhindi mmoja,” alisema Dk Nchimbi.
Kwenye operesheni hiyo alisema pia waliwakamata watuhumiwa 212 wa unyang’anyi pamoja na silaha mbalimbali zipatazo 61, baadhi zikiwa za kivita.

Alisema awamu ya pili ya operesheni ya kuwakamata wahamiaji haramu ipo mbioni ingawa alisema safari hii, idadi ya watakaounda timu ya uendeshaji wake itapungua.
Waziri huyo alisema kuwa wale wote wanaoishi nchini wanaweza kuamua kuondoka, kufanya mkakati wa kuomba uraia au kuwa na hati ya kusafiria pamoja na kibali cha kuwaruhusu kuishi nchini.
Chanzo:Mwananchi

No comments:

Zilizosomwa zaidi