Jeshi
la Polisi la Uturuki limetoa ufadhili wa masomo kwa askari kumi na
saba ( 17) wa Jeshi la Polisi Tanzania kupata mafunzo mbalimbali
yakiwemo ya upelelezi wa wahalifu na mbinu za uchunguzi wa kimaabara
pamoja na usimamizi na uendeshaji wa gari la matukio yatakayochukua muda
wa mwezi mmoja nchini Uturuki.
Mkurugenzi
wa Upelelezi wa makosa ya jinai nchini (DCI) Kamishina Robart Manumba
aliyasema hayo jana wakati wa kikao cha kazi kilichofanyika Makao Makuu
ya Polisi.
Alisema
kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya maboresho yanayolenga kuwaongezea askari
weledi na kuwajengea uwezo wataalamu wa Maabara ya uchunguzi ya Polisi
juu ya mbinu mbalimbali za kiuchunguzi na upelelezi pamoja na matumizi
sahihi ya vifaa vya kiupelelezi.
Aliongeza
kuwa mafunzo hayo yatasaidia wataalamu wa Maabara ya uchunguzi ya
Polisi kuweza kufanikisha kuwakamata wahalifu na kutambua uhalifu
uliotendeka kwa haraka, hivyo, kupunguza uhalifu nchini.
Kwa
upande wake Mkuu wa Maabara ya uchunguzi ya Jeshi la Polisi Naibu
Kamishina wa Polisi, (DCP) Abdularahaman Kaniki alisema kuwa mafunzo
hayo ni muendelezo wa ushirikiano uliopo baina ya Jeshi la Polisi
Tanzania na Jeshi la Polisi la Uturuki ambao ulianza katika mafunzo ya
upelelezi na ukusanyaji wa vielelezo katika eneo la tukio uliofanyika
hapa nchini mwishoni mwa mwezi juni mwaka huu.
Aidha,
aliwataka askari waliochaguliwa kushiriki mafunzo hayo kutumia fursa
hiyo kujifunza kwa bidii ili kuongeza ufanisi pamoja na kuboresha
utendaji katika maeneo mbalimbali ya upelelezi na Maabara ya
uchunguzi ya Polisi ili kufanikisha utambuzi wa uhalifu na wahalifu kwa
haraka.
No comments:
Post a Comment