Serikali imeziomba nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kuipa taarifa ya mikutano waliyoifanya bila ya kuishirikisha hivi karibuni.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe akizungumzia na waandishi wa habari ofisini
kwake jana alisema wameziomba nchi hizo kuitaarifu kile walichokijadili.
Alisema kwakuwa nchi hizo ni miongoni mwa nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zilitakiwa kutoa maelezo kwa
Umoja huo ili kila nchi wanachama ziweze kutambua lengo lao.
Membe alisema pia Serikali ya Tanzania, imeziomba
nchi hizo kuwapa maelezo ya kile walichokuwa wakikijadili katika mkutano
wao wa hivi karibuni uliofanyika Kenya.
“Tumewaomba wenzetu hawa, kutueleza mkutano wao
ulikuwa unahusu nini, kwani tulipaswa kujua kutokana na kuwa wanachama
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hata kama hawakutaka kutushirikisha,”
alisema Membe na kuongeza: “Nawaomba Watanzania wenzangu wasiwe na
wasiwasi juu ya mkutano huo, kwani tuna kila kitu hapa nchini. Hatuna
haja ya kuanza kufikiri mambo ambayo hayana msingi wowote.”
Alisema uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda
umeanza kuimarika baada ya marais wa nchi hizo, Jakaya Kikwete na Paul
Kagame, kukubaliana kuanza mazungumzo yatakayokuwa yakifanyika katika
nchi hizo.
Membe alisema Rais Kikwete na Rais Kagame,
walikutana peke yao, wakiwa na lengo la kuelezana na kuelimishana mambo
mbalimbali na walikubaliana kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo
mbili.
“Rais Kikwete amesema mkutano ulikuwa mzuri,
wamezungumza mambo mengi na wamekubaliana kuanza kufanya mazungumzo
yatakayokuwa yakifanyika Tanzania na Rwanda, hii itakuwa ni kuimarisha
uhusiano wetu na wao,” alisema Membe.
“Hali hii inakata majungu, uongo na fitna
zilizokuwa zikienezwa na watu, ambavyo vingeweza kusababisha
kutokuelewana baina yetu na wenzetu wa Rwanda.”
Alisema katika mkutano huo, marais hao
walielezana, kuchambua na kujadili ukweli, lengo likiwa ni kurudisha
uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
No comments:
Post a Comment