Friday, March 29, 2013

UNAJUA ATHARI ZA MARASHI NA SABUNI KWA MWANAMKE?...SOMA HAPA UJUE YALIYOMO.

Wanawake ni miongoni mwa wanajamii wengi wanaopenda kutumia marashi na vitu vingine kama sabuni zenye kemikali kwa ajili ya kujirembesha.
Pia, wanawake wamekuwa wakipenda usafi wao binafsi, wakitumia vitu  ambavyo baadhi yake ni hatari.
Wapo baadhi ya wanawake wanaopenda kusafisha sehemu zao za siri kwa kutumia sabuni zenye kemikali, marashi (pafyumu) au kupaka mafuta.
Kwa maelezo ya wataalam, hao wapo hatarini kupata magonjwa ya zinaa au ya kuambukiza.
Watafiti katika Chuo Kikuu cha California, Marekani wanasema sabuni ngumu au hata za maji, pafyumu (deodorant) zinaharibu tishu muhimu zilizomo ndani kabisa ya uke na kumweka mhusika katika hatari ya kupata malengelenge, fangasi  na hata Ukimwi.
Aidha, sabuni au dawa zinazouzwa na wafanyabiashara zikitangaza kuboresha uke au kuondoa harufu kwenye sehemu hizo nyeti nazo zimeelezwa kuwa na madhara.

 Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Cyriel Massawe anasema sabuni au mafuta yenye kemikali  huchubua  ngozi laini ya uke na ni rahisi vimelea vya magonjwa kuenea kwa urahisi.
Dk Massawe anasema michubuko hiyo ambayo si rahisi kuonekana kwa macho ndicho chanzo cha kuingia kwa maradhi ya kuambukiza.
“Hamna haja ya kuweka kemikali, au pafyumu ukeni. Hizo sehemu zinahitaji kuoshwa vizuri kwa maji,” anasema Dk Massawe.
Anasema kemikali inapoingia ukeni inavuruga hali ya kawaida na asidi inayolinda sehemu hizo.
Anaongeza  kuwa ni vyema wanawake wakaelimishwa kuhusu matumizi ya  bidhaa zinazodaiwa kuweka harufu nzuri  katika sehemu zao za siri, kurudisha bikira au mafuta ya kulainisha uke.
Naye Daktari Bingwa wa Kitengo cha Patholojia MNH, Henry Mwakyoma anasema wanawake wanaofanya usafi sehemu zao za siri kwa kutumia bidhaa au baadhi ya vifaa visivyofaa kutumiwa ukeni huweza kupata saratani ya shingo ya uzazi.
Dk Mwakyoma aliyewahi kufanya utafiti kuhusu saratani ya shingo ya kizazi nchini anasema, bidhaa zenye kemikali ya ‘coal tar,’ ambazo mara nyingine huwekwa kwenye sabuni ama manukato na kutumiwa ukeni na wanawake huweza kuchochea saratani hiyo.
Kiongozi wa utafiti huo, Dk Joelle Brown, alisema upo ushahidi wa kutosha kuwa kutumia sabuni za kuogea za maji au ngumu katika sehemu za siri za ndani za mwanamke kunaharibu uwiano wa bakteria na kusababisha bakteria kuzalishwa kwa wingi na kumweka mwanamke katika hatari ya maradhi ya  zinaa ya kuambukiza.
Chanzo:Mwananchi

No comments: