Thursday, March 21, 2013

17 WASIMAMISHWA KAZI TAZARA

Wafanyakazi 17 wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi baada ya kuhusishwa na tuhuma za kusafirisha mizigo kwa njia ya magendo kupitia treni ya uokoaji.
Mizigo hiyo ni mbao na mkaa iliyokuwa imehifadhiwa kwenye mabehewa sita ya treni hiyo, ikitokea eneo la Mzenga, wilayani Kisarawe, Pwani usiku wa kuamkia Jumapili.
Gharama za kusafirishia mizigo hiyo ilikuwa ni Sh12 milioni. Kaimu Mkurugenzi wa Tazara, Dk Damas Ndumbaro alisema hatua hiyo ni kupisha uchunguzi.

“Na kuanzia leo (jana), tutakapothibitisha wamehusika wote tunawafukuza kazi, huo ndiyo uamuzi tuliofikia kwa sababu hatuwezi kuendelea kukaa na watu wanaokwenda kinyume na mipango yetu,” alisema Dk Ndumaro.

Pia, Dk Ndumaro alisema hivi sasa mamlaka hiyo imeandaa mpango wa kufanya mabadiliko kuanzia utawala, kuongeza mtaji na kuweka utaratibu wa uwajibikaji kwa viongozi.

“Ili kuifanya Tazara nyingine kuna makubaliano ya mkataba kwa wafanyakazi, kiongozi anasaini kutimiza majukumu kadhaa ndani ya kipindi fulani kama sehemu ya makubaliano, akishindwa lazima awajibike mwenyewe,” alisema Dk Ndumbaro.

Dk Ndumaro alisema iwapo mamlaka itafanikiwa, uzalishaji utapanda kutoka tani 60,000 za mizigo hadi 80,000 kwa mwezi, hatua itakayoongeza kasi mzunguko wa fedha.
“Kiwango tunachoingiza kwa sasa ni dola 4 milioni za Marekani, lakini tutakapofanikiwa bajeti hiyo tutaweza kufikia dola 6 milioni ukilinganisha na matumizi yetu siyo chini ya dola 3 milioni,” alisema

Taarifa zinaonyesha utendaji umeporomoka kwa kiwango kikubwa, kwani tangu bajeti ya mwaka 1986/87 mamlaka ilikuwa inasafirisha tani za mizigo 1.2 milioni na abiria wasiopungua milioni moja, lakini mwaka wa fedha wa 2011/12 mamlaka hiyo imeshuka kwa kiwango cha tani za mizigo 340,000 na abiria wasiozidi 900,000.

No comments:

Zilizosomwa zaidi