MWAKA 1848, Mmishenari wa Kijerumani Dk Johan Ludwig Krapf,
alitembelea kijiji cha Magila kilichopo Muheza mkoani Tanga akiwa
katika safari zake za Afrika Mashariki.
Magila kuna mlima ulio katika safu za milima ya
Usambara ukipakana na mlima wa Magoroto ambao ndio chanzo cha maji ya
mto Mkurumuzi unaoelekea Muheza.
Historia inaonyesha eneo la mlima Magila wenye
miamba na mawe mengi, zamani kabla ya kuja wageni lilitumika kuwatenga
wagonjwa wa ukoma na magonjwa mengine yasiyotibika, kwa lengo la
kuwazuia wasiwaambukize wengine.
Dk Krapf alipofika na kuwaona wagonjwa hao
waliokuwa wakiishi kwa madhila makubwa, alichonga msalaba katika mti wa
mkuyu kwa imani kuwa Mwenyezi Mungu angewaponya wagonjwa hao.
Eneo hilo ndilo lililokuja kujengwa shule ya
kwanza na Waingereza mwaka 1886. Alama ya msalaba huo ipo hadi na sasa
na ndipo ilipo Shule ya Sekondari Hegongo.
Hadi leo mahali hapo panaitwa Magila Msalabani.
Kwa sasa Magila ni kata yenye vijiji vya vya Magila, Mikwamba, Misongeni
na Mafleta.
Nilifika katika eneo hilo nilipokuwa wilayani Muheza hivi karibuni ili kuchunguza historia ya eneo hilo.
Hapo nikutana na Luteni Kanali mstaafu John Mhina
ambaye amekamilisha kuandika kitabu kuhusu historia ya Magila Msalabani,
kinachoeleza historia ya kijiji hicho na ujio wa wazungu walioanzisha
shule ya kwanza Tanganyika na kanisa.
Luteni Kanali Mhina aliyelitumikia Taifa kwa muda
mrefu kama mwanajeshi , na baadaye kuwa Mbunge wa Muheza kutoka mwaka
1990 hadi 1995, anasema harakati za kuanzisha shule katika kijiji hicho
zilitokana na Wamishenari waliokuja Afrika Mashariki kutoka Ulaya
kwaajili ya kueneza dini ya kikristo tangu miaka ya 1770.
Anawataja baadhi ya Wamishenari hao kuwa ni pamoja na David Livingstone, Charles Mackenzie, William Tozer na Edward Steer.
Anasema harakati hizo zilianzia tangu visiwa vya
Zanzibar mwaka 1863 ambako pia walikomesha biashara ya utumwa na kuanza
ujenzi wa kanisa la Anglikana la Mkunazini Zanzibar kwa miaka 10 tangu
mwaka 1873.
Anasema wakati huo kulikuwa na shule iliyoanzishwa
Zanzibar maeneo ya Kiungani na Kiinua mguu na Askofu William Tozer
mwaka 1869. Hata hivyo, anasema shule hiyo haikuwa rasmi na ilikuwa
ikifundisha elimu ya dini kwa watumwa waliokombolewa.
CHANZO. MWANANCHI
CHANZO. MWANANCHI
No comments:
Post a Comment