WAKATI Bunge likianza mkutano wake wa Tisa leo, zipo taarifa kuwa ripoti ya
Kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza tuhuma za wabunge kujihusisha na
vitendo vya rushwa haitasomwa na kisha kujadiliwa.Badala yake Kamati ya Uongozi, iliyokutana jana iliamua kwamba litatolewa tamko kuhusu ripoti ya kamati hiyo, hivyo haitasomwa wala kujadiliwa kama ambavyo wabunge wamekuwa wakitaka.
Kwa maana hiyo Spika wa Bunge, Anne Makinda huenda akatumia kanuni nyingine kutoa tamko kuhusu uchunguzi huo, hali ambayo haitatoa fursa kwa wabunge kuijadili kama ambavyo baadhi yao wamekuwa wakishinikiza.
Miongoni mwa kanuni ambazo Spika anaweza kuzitumia ni pamoja na ile ya 33 (2) ambayo inasema: “Wakati wa kikao, Spika anaweza kutoa taarifa nyinginezo kadri atakavyoona inafaa.”
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel jana alikataa kuzungumzia suala hilo akiahidi kulitoa ufafanuzi leo... “Ratiba ya shughuli za Bunge bado iko kwenye ngazi ya Kamati ya Uongozi. Sasa pengine tusubiri kesho (leo) ikiwa tayari kila kitu kitakuwa wazi, hakuna haja ya kuwa na haraka.”
No comments:
Post a Comment