Tuesday, October 2, 2012

Kada wa Chadema amtishia Kikwete/



KADA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Amani Mgheni amemtahadharisha Rais Jakaya Kikwete kuwa asipokuwa makini katika kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za Taifa ataandika historia ya kuwa rais wa kwanza kushtakiwa mahakamani kwa kushindwa kusimamia rasilimali hizo.
Mgheni ambaye ni Katibu wa Jimbo la Segerea wa Chadema, alitoa tahadhari hiyo wakati akitoa salamu kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika mtaa wa Ugombolwa, Kata ya Segerea, jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa kama Rais Kikwete asipowachukulia hatua za kisheria kwa kuwafikisha mahakamani watendaji wanaotuhumiwa kutumia vibaya rasilimali za umma, chama chake kikiingia madarakani atahakikisha anashtakiwa.
“Haiwezekani rasilimali za umma zinatumiwa vibaya, kama vile wanyama kutoroshwa kwenda nje ya nchi, lakini watuhumiwa wanaachwa tu bila kuchukuliwa hatau za kisheria,” alisisitiza Mgheni na kuongeza:
“Kama rais  asipowachukulia hatau za kisheria, maana yake ni kwamba  anajua kilichokuwa kinaendelea, hivyo kwa kuwa yeye ndiye aliyewateua, basi, 2015 ataweka historia ya kuwa rais wa kwanza kusimama kizimbani kujibu tuhuma za kushindwa kusimamia vizuri rasilimali za umma.”.
 Diwani wa Kata ya Segerea, Azuri Mwambagi aliwataka wananchi kujitokeza kuhudhuria mikutano mbalimbali ya Serikali za Mitaa ili kuhakikisha kwamba kamati mbalimbali zinazoundwa kusimamia shughuli za maendeleo zinakuwa imara.
Alisema kuwa bila kuwa na serikali za mitaa imara na kamati zisizoundwa kutokana na matakwa ya watu wachache tu, ni vigumu kupata maendeleo.
Akizungumzia utendaji kazi wake tangu alipochaguliwa, Mwambagi alisema kuna mambo mengi aliyokwishayafanya na mengine yako katika mchakato, huku akilalamika kuwa juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi zimekuwa zikipigwa vita na baadhi ya viongozi katika Manispaa ya Ilala.
“Mimi nimekuwa nikihangaika mchana na usiku kutatua kero za wananchi, lakini kuna watu wengine wananipiga vita. Wananchi ni lazima tushikamane,”  alisema Mwambagi.
Alifafanua kuwa wakati alipochaguliwa kuwa diwani, barabara za katahiyo ilikuwa katika hali mbaya na kwamba aliazimia kuwa barabara hizo zitakuwa zinachongwa kila mwaka na kuwekwa katika kiwango cha moramu ili ziweze kutumika kwa urahi kwa mwaka mzima.
Hata hivyo alibainisha kuwa kuna wakati alipeleka greda kuchonga barabara katika kata hiyo lakini alitumiwa ujumbe na kiongozi mmoja akihoji mahali lilikotoka greda hilo kama ni la Chadema au la Serikali, akidai kuwa yeye hana taarifa nalo.
“Hata hivyo nimeamua kuwa barabara zitakuwa zinachongwa kila mwaka ili ziweze kupitika kwa urahisi,” alisisitiza Diwani Mwambagi.

No comments:

Zilizosomwa zaidi