Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa utaratibu wa
kushughulikia malalamiko ya wanafunzi wanaopata mikopo katika taasisi
za elimu ya juu nchini.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es salaam na Meneja wa Habari, Elimu na
Mawasiliano Omega Ngole alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu
utaratibu wa kushughulikia malalamiko ya wanafunzi wa elimu ya juu
nchini.
“Utaratibu
huu ulioboreshwa, ni msisitizo na maelekezo ya Serikali ya mwezi Agosti
2011 kupitia iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo
ilielekeza Taasisi zote za Elimu ya Juu nchini zinazopata mikopo kutoka
Bodi ya Mikopo kuanzisha Madawati ya Mikopo ili kuongeza ufanisi katika
utoaji mikopo”,Alisema Ngole.
Ameongeza
kuwa, dawati hilo linatakiwa kusimamiwa na mtumishi teule wa chuo
husika mwenye sifa na uhusiano mzuri na jamii na linapaswa kuwa chini ya
Makamu Mkuu wa chuo husika anayeshughulikia taaluma.
Meneja wa
Habari , Elimu na Mawasiliano Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB)
Bw. Omega Ngole akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani kuhusu
utaratibu wa kushughulikia malalamiko ya wanafunzi kuhusu upatikanaji wa
mikopo elimu ya juu uliofanyika Jijini Dar es salaam.
Meneja
Ngole amesisitiza kuwa kwa sasa vyuo vyote vina Maofisa Mikopo ambao
wanawajibika kutafuta suluhisho la suala linalowasilishwa na kulitolea
majibu.
Akifafanua
hatua zinazotakiwa kufuatwa na Maofisa hao katika kutafuta suluhisho la
malalamiko ya wanafunzi amesema kuwa, baada ya malalamiko kufika kwa
Ofisa Mikopo yanatakiwa yapate suluhisho ndani ya siku mbili tangu
kuwasilishwa kwake,ikiwa hatakua na ufumbuzi atatakiwa kuwasiliana na
uongozi wa juu wa chuo husika.
Endapo
uongozi wa juu wa chuo hautokuwa na ufumbuzi, malalamiko hayo
yatatakiwa kupelekwa kwenye Ofisi za Kanda ambazo zinapatikana katika
Mikoa ya Mwanza, Dodoma, Arusha na Zanzibar au ofisi za makao ya makuu
ya Bodi zilizoko jijini Dar es Salaam.
Bodi ya
Mikopo ilianzishwa kwa sheria ya Bunge namba 9 ya mwaka 2004 na kuanza
rasmi mwezi Julai 2005 kwa majukumu ya kutoa mikopo kwa wanafunzi
wahitaji waliodahiliwa katika Taasisi za Elimu ya Juu pamoja kukusanya
marejesho ya mikopo yote iliyotolewa tangu mwaka 1994.
No comments:
Post a Comment